1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Niger lazuia mashambulizi ya Boko Haram

6 Mei 2020

Jeshi la Niger limezuia mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Boko Haram mjini Diffa. mji huo ulio na wakaazi 200,000 umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na kundi hilo tangu lilipoanza uasi mwaka 2009.

https://p.dw.com/p/3brLw
Symbolbild | Nigeria | SWAT
Picha: Imago Images/ZUMA Press/Planetpix/A. F. E. Lii

"Tulisikia milio ya risasi kati ya saa kumi alasiri na saa moja usiku katika eneo la kusini mwa mji huu. Lilikuwa ni shambulizi la Boko Haram waliojaribu kuingia huku”, Lawan Boukar mmoja wa wakaazi wa Diffa aliliambia shirika la habari la AFP.

Chanzo kimoja cha usalama kimethibitisha shambulizi hilo lakini hakutoa maelezo zaidi. Yamkini wizara ya ulinzi imesema itatoa taarifa baadaye kuhusu shambulizi hilo.

Eneo hilo la Diffa pamoja na Chad ambayo zinapakana na Nigeria zimekuwa zikishambuliwa na wanamgambo wa Boko Haram tangu mwaka 2015. Kundi hilo lina maficho yao karibu na ziwa Chad linalounganisha Cameroon, Chad, Niger na Nigeria.

Niger yadai kumuua mmoja wa viongozi wa Boko Haram

Nigerianische Rebellen Niger Delta
Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Osodi

Shambulizi hilo la Jumapili linaonekana kama shambulizi la kulipiza kisasi baada ya Chad kufanya shambulizi la anga na la ardhini dhidi ya kundi la Boko Haram baada ya kundi hilo kuwashambulia na kuwaua wanajeshi wapatao 100 wa Chad. Chad inadai kuwa iliwaua maelfu ya wapiganaji wa Boko Haram na kuwafukuza kutoka ngome zao.

Mnamo mwezi Machi wizara ya ulinzi ya Niger ilidai kuwa Ibrahim Fakoura ambaye ni mmoja kati ya viongozi wakuu wa Boko Haram aliuawa katika oparesheni ya kijeshi iliyofanyika katika eneo la ziwa Chad.

Mwaka 2015, mapigano makali yalizuka kati ya wanajeshi wa Niger na wapiganaji wa Boko Haram karibu na daraja la kimkakati la Doutchi na kijiji cha Damasak, ambacho kilikuwa chini ya udhibiti wa wapiganaji hao tangu mnamo mwezi Oktoba 2014. Kijiji hicho cha Damasak sasa kiko chini ya himaya ya jeshi la Niger baada ya ushirikiano na wanajeshi wa Chad kuwatimua Boko Haram kijijini humo.

Chanzo: afp