Jeshi la Nigeria laonya juu ya maandamano ya vurugu
26 Julai 2024Jeshi la Nigeria limesema limejiandaa kukabiliana na uvunjaji wowote wa sheria.
Rais Bola Ahmed Tinubu amesema katika taarifa kuwa hawaogopi maandamano bali wasiwasi wao ni kuhusu usalama wa raia na uharibifu ambao huenda ukatokea.
Kiongozi huyo ametoa mwito kwa raia wa nchi hiyo kuwa waangalifu na kuonya juu ya kuigeuza Nigeria kuwa kama Sudan, akiashiria vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 15 katika nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika.
Soma pia: Nigeria kuendelea na mageuzi ya kiuchumi
Maafisa wa serikali, vikosi vya usalama na magavana nchini Nigeria wamewarai vijana kujiepusha na maandamano. Baadhi ya viongozi wameshtumu waandaaji wa maandamano hayo kwa uhaini na kuwa na nia ya kuliyumbisha taifa.
"Wakati raia wana haki ya kuandamana kwa amani, hawana haki ya kuhamasisha machafuko na kusababisha ugaidi," msemaji wa wizara ya ulinzi ya Nigeria Meja Jenerali Edward Buba amewaambia waandishi wa habari.
Msemaji huyo amefahamisha kuwa jeshi limegundua baadhi ya watu wanaopanga kuteka nyara maandamano hayo.
"Kiwango cha vurugu kinachoweza kutokea kitatafsiriwa kama uvunjaji wa sheria. Vikosi vya jeshi kwa upande wake havitasimama tu na kuruhusu hali ya machafuko kulikumba taifa letu."
Kenya ilikumbwa na maandamano makubwa yaliyoilazimu serikali kutupilia mbali mswada tata wa fedha uliotoa mapendekezo ya kuongeza ushuru. Mageuzi ya kiuchumi ya Nigeria yameshuhudia ongezeko la asilimia 40 ya mfumuko wa bei ya vyakula.
Soma pia: Maandamano Kenya yatatiza shughuli katika uwanja wa ndege
Kumetolewa miito katika mitandao ya kijamii kwa Wanaigeria kufanya maandamano kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha kuanzia Agosti mosi.
Hata hivyo haijabainika ni kina nani hasa wanaochochea maandamano hayo au hata iwapo watu watajitokeza barabarani hasa wakati huu ambapo raia wengi wa Nigeria wana hofu juu ya kupoteza kazi zao au uwoga wa kukamatwa.