1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Jeshi la Sudan lagoma kusitisha mapigano wakati wa Ramadhan

10 Machi 2024

Jeshi la Sudan limesema hakutakuwa na makubaliano ya usitishaji mapigano wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan hadi pale wanamgambo wa RSF watakapoondoka kwenye makazi na maeneo ya raia.

https://p.dw.com/p/4dMT4
Kituo cha Renk | Wakimbizi wa Sudan waliokimbia mzozo nchini mwao
Wakimbizi wa Sudan waliokimbia vita nchini Sudan wakishuka kwenye lori lililobeba familia zinazowasili katika Kituo cha muda cha wakimbizi huko Renk, Februari 13, 2024. Zaidi ya watu 550,000 sasa wamekimbia vita nchini Sudan na kuelekea Sudan Kusini.Picha: LUIS TATO/AFP

Afisa wa ngazi za juu wa vikosi vya jeshi la Sudan Jenerali Yasser al-Atta amesema hayo leo katika taarifa kupitia mtandao wa Telegram, baada ya wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa usitishwaji wa mapigano wakati wa Ramadhan inayotarajiwa kuanza wiki hii.

RSF iliukaribisha wito huo wa Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya Atta iliyoangazia hatua za hivi karibuni za jeshi katika mji wa Omdurman, unaochukua sehemu kubwa ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum, imesisitiza kwamba hawatasitisha mapigano hadi RSF watakapotimiza ahadi waliyoitoa Mei mwaka uliopita wakati wa mazungumzo yaliyosimamiwa na Saudi Arabia na Marekani mjini Jeddah ya kuondoka kwenye maeneo hayo.