Jeshi la Sudan lasema vikosi vyake vimeondoka Wad Madan
19 Desemba 2023Hatua ya wanamgambo wa RSF kuchukua udhibiti wa sehemu ya kati na maeneo mengine ya mji wa Wad Madani unaowahifadhi wahamiaji wengi na ambao pia ni kitovu cha misaada kwa sasa hivi, huenda inaweza kuwa mwanzo wa wanamgambo hao kusonga mbele zaidi hadi miji ya magharibi na maeneo ya kati ya Sudan.
Mji huo uko umbali wa takriban kilomita 170 kusini mashariki mwa mji mkuu Khartoum katika jimbo la El Gezira, eneo ambalo ni muhimu kwa shughuli za kilimo lakini katika nchi inayokabiliwa na njaa inayozidi kuwa mbaya.
Kupitia taarifa, shirika la wahamiaji IOM limesema kati ya watu 250,000-300,000 walikuwa wamekimbia El Gezira tangu mapigano yalipoanza siku nne zilizopita.
Video zilizosambazwa na wanamgambo wa RSF mitandaoni ziliwaonesha wapiganaji wakiendesha magari kwenye mitaa ya Wad Madani na wakiwa kwenye daraja muhimu la mto Blue Nile ambalo walikuwa wakipigania udhibiti wake dhidi ya jeshi. Mashuhuda wamesema wanamgambo hao pia walivamia vijiji vilivyoko karibu.
Katika video moja, wapiganaji wa RSF waliokuwa wamebeba bunduki walisimama wakiwazunguka makuhani wa kanisa la Coptic, ambao walisema hawakuweza kukimbia lakini waliomba msaada wa RSF waweze kuondoka jijini.
Hata hivyo shirika la Habari la Reuters halikuweza kuthibitisha video hizo. Nalo jeshi la Sudan halikuzungumzia video hizo.
Soma pia: Wanamgambo wa RSF wachukua sehemu ya mji wa Wad Madani
Wanaharakati wa ndani wanaounga mkono demokrasia walisema kikosi cha RSF kilikuwa kimeanzisha vituo vya ukaguzi katika jiji lote na walikuwa wakipora nyumba na magari, bila jeshi wala polisi kuwepo.
Wakati watu nusu milioni walikuwa wamekimbilia eneo kubwa Zaidi la jimbo la El Gezira, takriban 85,000 walikuwa wakiishi ndani ya mji wa Wad Madani, kwa kutegemea zaidi huduma za afya za mji huo, misaada na vilevile huduma za serikali zilizoanza kuzimwa siku za hivi karibuni.
Reem Abbas, mtafiti katika taasisi ya Tahrir amesema kuchukua udhibiti wa Wad Madani, ambao pia unaunganisha barabara kuu, kutaipa RSF udhibiti mkubwa wa biashara na kuiruhusu kudhibiti njia ambazo jeshi hutumia kwa usambazaji wake wa vifaa.
Aidha ameongeza kuwa udhibiti huo unawapa wanamgambo muda wa kujipanga, na wanaweza kwenda mashariki na kuendelea kuwashikilia watu mateka, ili kuweka shinikizo kwa jamii, kwa jeshi, na jumuiya ya kimataifa.
Mnamo Jumapili, Marekani iliitaka RSF isiushambulie mji wa Wad Madani. Marekani na Saudi Arabia zimekuwa zikiongoza juhudi za upatanishi kusuluhisha mgogoro huo wa Sudan, lakini hakujakuwa na suluhisho la kudumu.
Soma pia: Mapigano mapya yazuka kusini mwa Sudan
Wapatanishi wa kikanda IGAD, wamesema jeshi la Sudan na RSF walikubaliana kusitisha mapigano wiki iliyopita. Lakini muda mfupi baadaye pande zote mbili zilijitenga haraka na madai hayo.
Vita kati ya wanamgambo wa RSF wanaoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo na jeshi la kitaifa linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan vimedumu kwa zaidi ya miezi minane sasa.
Pande hizo mbili ziliwahi kugawana mamlaka na raia baada ya mapinduzi ya mwaka 2019 yaliyouangusha uliokuwa utawala wa Rais Omar al-Bashir. Baadaye mwaka 2021, walifanya mapinduzi tena na kuanza kuzozana kuhusu mpango wa kisiasa wa mpito unaoungwa mkono kimataifa.
Tangu machafuko hayo yalipoanza, zaidi ya watu milioni saba wameyakimbia makaazi yao na maafa mengine makubwa pia yametokea.