1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Jeshi lachukua udhibiti wa Bangladesh

6 Agosti 2024

Mkuu wa majeshi la Bangladesh anatarajiwa kukutana leo na viongozi wa maandamano ya wanafunzi, siku moja baada ya jeshi kuchukua udhibiti wa nchi.

https://p.dw.com/p/4j9j4
Bangladesch | Dhaka | Jeshi likiwa mitaani na waandamanaji.
Wanajeshi wakishangiliwa na vijana waandamanaji BangladeshPicha: Mohammad Ponir Hossain/REUTERS

Maandamano makubwa yalimlazimu mtawala wa muda mrefu, Sheikh Hassina, kukimbilia uhamishoni. Mkuu wa majeshi Jenerali Waker-Uz-Zaman alitangaza jana kwenye televisheni ya taifa kuwa Hasina amejiuzulu na jeshi litaunda serikali ya mpito.

Viongozi wa maandamano ya wanafunzi, kabla ya mkutano wao na mkuu wa majeshi leo, wamesema wanamtaka mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel na muasisi wa sekta ya mikopo kwa wafanyabiashara wadogowadogo nchini humo, Muhammad Yunus, kuiongoza serikali hiyo. Yunus ana umri wa miaka 84.

Nahid Islam ni mratibu wa vuguvugu la wanafunzi alimesema wameamua kwamba serikali ya mpito itaundwa, itakayoongozwa na mshindi wa Tuzo ya Nobel anayekubalika kimataifa, Dk Muhammad Yunus.

Soma pia:Wanafunzi wapendekeza mshindi wa Nobel kuwa Waziri Mkuu Bangladesh

"Tulizungumza na Muhammad Yunus pia. Amekubali kuchukua jukumu hili kuokoa Bangladesh, akiitikia wito wa wanafunzi na wa umma."

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa zamani wa Bangladesh Khaleda Zia ameachiliwa huru kutoka miaka mingi ya kifungo cha nyumbani. Msemaji wa chama chake cha Bangladesh National Party - BNP amethibitisha hilo siku moja baada ya amri ya kutaka aachiwe kutolewa wakati jeshi lilipochukua udhibiti. Aidha vyombo vya habari nchini humo vikinukuu taarifa kutoka ofisi ya rais vimeripoti kuwa Bunge limevunjwa.

Hasina, mwenye umri wa miaka 76, amekuwa madarakani tangu 2009 lakini alituhumiwa kwa kuchakachua matokeo ya uchaguzi wa Januari hali iliyochochea mamilioni ya watu kuingia mitaani kwa mwezi mzima kudai ajiuzulu.