Jeshi Myanmar lajiongezea miaka miwili madarakani
2 Agosti 2021"Lazima tutayarishe mazingira ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki unaoshirikisha vyama vingi. Tunapaswa kufanya matayarisho hayo. Naahidi kuitisha uchaguzi mkuu huo wa vyama vingi bila kuchelewa," alisema kiongozi wa baraza la kijeshi la Myanmar, Jenerali Min Aung Hlaing, kwenye hotuba yake iliyorushwa na televisheni ya taifa usiku wa Jumapili (Agosti 1), akisisitiza kwamba utawala wake wa hali ya dharura ungelifikia kikomo mwezi Agosti 2023.
Katika tangazo tafauti na hilo, baraza hilo la kijeshi lilijipa jina la "serikali ya mshiko" na kumteuwa Jenerali Min kuwa waziri wake mkuu.
Hali ya dharura ilitangazwa tangu jeshi lilipoipinduwa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Aung San Suu Kyi tarehe 1 Februari, hatua ambayo majenerali hao walidai inaruhusika kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2008 iliyoandikwa na jeshi lenyewe.
Jeshi lilidai kuwa ushindi wa kishindo alioupata Aung San Suu Kyi na chama chake kwenye uchaguzi wa bunge ulitokana na wizi mkubwa wa kura, ingawa halikutowa ushahidi wowote kuthibitisha madai yake.
Upinzani wa umma
Ililichukuwa jeshi hilo miezi sita kuyafuta rasmi matokeo ya uchaguzi huo Jumanne iliyopita na kuteuwa tume mpya ya uchaguzi.
Hata hivyo, mapinduzi hayo ya kijeshi ya Februari Mosi yamekumbana na upinzani mkali wa umma na kwenye matukio kadhaa upinzani huo umekabiliwa kwa matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola.
Kufikia jana Jumapili, watu 939 walikuwa wameshauwa na vyombo vya usalama tangu maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi kuanza, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na Jumuiya ya Wafungwa wa Kisiasa.
Waliopoteza maisha ni pamoja na maafisa wa kijeshi na polisi, kwani kumezuka makundi yenye silaha yanayounga mkono waandamanaji kwenye maeneo ya mijini na vijijini.
ASEAN yataka mjumbe aidhinishwe
Hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Indonesia, Retno Marsudi, aliuomba utawala wa kijeshi wa Myanmar kumuidhinisha mjumbe maalum wa Jumuiya ya Mataifa ya Asia ya Kusini na Mashariki, ASEAN, aliyeteuliwa kuushughulikia mzozo huo.
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa ASEAN walikutana siku ya Jumatatu (Agosti 2) mjini Jakarta kukamilisha mipango ya mjumbe huyo aliyepewa jukumu la kuitisha majadiliano ya kukomesha ghasia na kuyakutanisha makundi ya upinzani na serikali ya kijeshi.
Lakini, akizungumza na waandishi wa habari kupitia video, Marsudi alisema hadi sasa hawajapiga hatua yoyote ya maana kuelekea utatuzi wa mkwamo uliopo katika suala la Myanmar.