1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi Uganda latoa kanda ya vidio ya Bobi Wine akitabasamu

Lubega Emmanuel22 Agosti 2018

Kanda ya vidio ya sekunde nane ambayo imesambazwa na jeshi la Uganda latarajiwa kuondosha hofu kuhusu hali ya Bobi Wine, lakini baadhi wana tashwishi na uhalali wa kanda hiyo

https://p.dw.com/p/33bJQ
Uganda Kyagulanyi Ssentamu
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Wandera

Ukanda wa sekunde nane uliosambazwa na msemaji wa majeshi ya Uganda ukionyesha mbunge na msanii Bobi Wine akitabasamu wakati alipotembelewa na naibu wa spika hii leo umetarajiwa kuondosha hofu na mashaka kuhusu hali alimo bwana huyo.

Hatua hii pamoja na maombi maalum yaliyofanyika adhuhuri kwa lengo la kurejesha amani na maridhiano kati ya serikali na wakosaoaji wake ni miongoni mwa hali ambazo yamkini zimetuliza hisia za wafuasi wa mbunge huyo na mwenzake Francis Zake.

Hata hivyo wanahabari wametisha kuongoza maandamano ya amani kote nchini ikiwa jeshi halitatambulisha na kuwaadhibu waziwazi askari wake wakiowapiga wenzao na kuharibu vifaa vyao.

Ibada maalum ya kuombea amani Uganda baada ya siku nne za machafuko waandamanaji wakiitaka serikali kumwachia mbunge na msanii Bobi Wine pamoja na mwenzake Francis Zake imefanyika kwenye kanisa kuu la Katoliki mlimani Lubaga mjini Kampala. Watu wa tabaka mbalimbali wameshiriki katika maombi hayo wakielezea kuwa hii ni njia mojawapo ya kuleta utulivu kwa umma kuhusiana na mgogoro wa kisiasa uliozuka wiki iliyopita.

Maafisa wa usalama wa Uganda wakimkamata mwanamanaji mjini Kampala
Maafisa wa usalama wa Uganda wakimkamata mwanamanaji mjini KampalaPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Kabuubi

Uhalali wa kanda hiyo ya vidio watiliwa shaka

Wakati huo huo, hatimaye msemaji wa jeshi amesambaza ukanda wa video wa sekunde nane ukionyesha mbunge Bobi Wine akitembelewa na naibu spika wa bunge korokoroni anakozuiliwa katika kambi ya jeshi Makindye.

Waandishi habari walikatazwa kuandamana na naibu spika Jacob Oulanya na hii yumkini ndiyo sababu baadhi ya watu wamekataa kuamini kama ukanda huo ni wa Bobi Wine kama alivyo kwa sasa. lakini Naibu spika ameelezea kuwa mwanasiasa huyo amefurahi kuwaona japo amedhihirisha kuwa yumo katika maumivu makubwa.

Kwa upande wao waandishi habari wametisha kuongoza maandamano ya amani kote nchi ikiwa jeshi la Uganda, UPDF halitawatambulisha waziwazi askari wake waliowahujumu wenzao kwa mijeledi pamoja na kuharibu vifaa vyao.

Msemaji wa majeshi Brigedia Richard Karemire aliahidi kuwa jeshi litawaadhibu wahusika kwani vitendo vyao vilikuwa vya kufedhehesha na kukiuka mwongozo wa jeshi.

Hapo kesho mbunge Bobi Wine anatarajiwa kufika tena katika mahakama ya kijeshi kuhusiana na mashataka ya kupatikana na bunduki mbili na risasi katika chumba cha hoteli alimokuwa kule Arua wakati ghasia zilizotokea na dereva wake akapigwa risasi.

Mhariri: Josephat Charo