1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Kerry :Ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Israel sio halali

Admin.WagnerD6 Novemba 2013

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry yuko mashariki ya kati katika ziara inayonuia kuyapiga jeki mazungumzo kati ya Israel na Palestina yanayoonekana kuyumbayumba

https://p.dw.com/p/1ADFS
Picha: Reuters

Kerry ambaye ndiye mpatanishi mkuu kati ya Israel na Palestina amesema panda shuka zinazoshuhudiwa zinatarajiwa kama katika mazungumzo yoyote yale, lakini ana imani kuwa vikwazo vilivyoko vitakabiliwa na kuleta amani ya kudumu katika kanda hiyo ya mashariki ya kati.

Kerry aliyasema hayo leo mjini Bethlehem alikokutana na rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, baada ya mkutano na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjini Jerusalem.

Waziri huyo wa Marekani amesema ana hakika kuwa licha ya matatizo, viongozi wote wawili wa mamlaka ya ndani ya Palestina Abbas na wa Israel Netanyahu wana nia ya kuafikia ufumbuzi wa mzozo huo.

Licha ya tamko hilo lililojaa matumaini kutoka kwa Kerry, uhasama unazidi kutokota kati ya pande hizo mbili husika.

Vuta nikuvute yazidi mashariki ya kati

Huku Palestina hapo jana ikitishia kujiondoa kutoka kwa mazungumzo kufuatia azma ya Isreal ya kuendelea na mpango wa kujenga makaazi mapya ya walowezi katika eneo linalozozaniwa, Waziri mkuu wa Israel amewashutumu wapalestina kwa kubuni mzozo usiokuwepo na kutatiza mazungumzo.

Makaazi mapya ya walowezi ya Israel katika ukingo wa magharibi
Makaazi mapya ya walowezi ya Israel katika ukingo wa magharibiPicha: picture-alliance/dpa

Palestina imeghadhabishwa na kuendelea kwa Israel kujenga makaazi mapya ya walowezi, jambo ambalo Netanyahu anasisitiza halikuweko kama sharti kutoka kwa Palestina wakati mazungumzo hayo yalipofufuliwa miezi mitatu iliyopita na badala yake, Palestina ilitaka kuachiwa kwa wafungwa 104 ili ishawishike kurejea katika meza ya mazungumzo.

Kerry amesema leo kuwa msimamo wa Marekani ni kuwa ujenzi wa Israel ni kinyume na sheria na kwamba Palestina haikukubaliana na ujenzi huo tangu mwanzo.Hii ni mara ya kwanza kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani kutamka msimamo wazi kuhusiana na suala hilo tete.

Pande zote zahimizwa kurejea katika meza ya mazungumzo

Kerry amesema wamesalia na miezi sita kuambatana na ratiba ya kukamilisha mazungumzo na kukubaliana; mpango uliofikiwa mwezi Julai kuweza kupiga hatua zinazohitajika ili ifikapo Aprili mwakani yawe yamekamilika.

Pande hizo mbili pia zinatofautiana kuhusu hatma ya Jerusalem na bonde la Jordan ambayo ni asilimia 40 ya Ukingo wa Magharibi ambako Israel inataka kuendelea kuweka majeshi yake huko hata baada ya makubaliano ya amani iwapo yataafikiwa.

Abbas siku ya Jumatatu amesema Palestina haitakubali kuachia hata milimita moja ya ardhi yake mashariki mwa Jerusalem ambako kunatarajiwa kuwa makao makuu ya utawala ujao wa Palestina wala kuruhusu bonde la Jordan kukaliwa kijeshi na Israel.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John KerryPicha: picture-alliance/dpa

Mshauri wa Abbas, Nimr Hammas, amedokeza kuwa Palestina haina nia ya kujiondoa katika mazungumzo lakini akaongeza anatarajia Marekani kuchukua msimamo mkali kama uliochukuliwa na Umoja wa Ulaya kupinga ujenzi wa makaazi mapya ya walowezi na Israel na sio kuegemea upande wowote katika mzozo huo.

Akiwa mjini Bethlehem, Kerry ametangaza kuwa Marekani itatoa msaada zaidi wa dola milioni 75 kubuni nafasi za ajira kwa Wapalestina na kuboresha mabarabara, mashule na miundo mbinu.

Akimaliza mazungumzo na Abbas, Kerry anatarajiwa kurejea Jerusalem kwa mkutano na rais wa Israel, Shimon Peres, na baadaye jioni kuwa na dhifa ya chakula na Netanyahu.

Hapo kesho anapanga kusafiri kuelekea Jordan ambako anatarajiwa kukutana tena na Abbas kwa awamu nyingine ya mazungumzo.

Mwandishi:Caro Robi/ap/dpa

Mhariri: Josephat Charo