1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Terry kizimbani kwa madai ya kibaguzi

9 Julai 2012

Kesi ya madai ya ubaguzi wa rangi inayomkabili John Terry imeanza huku waendesha mashitaka wakidai kuwa nahodha huyo wa Chelsea anakiri alitumia lugha chafu kuelezea mshangao wa kejeli wakati wa majibizano uwanjani.

https://p.dw.com/p/15UCs
John Terry mit KapitänsbindePicha: dapd

Beki huyo wa Uingereza alikutana ana kwa ana mahakamani na beki wa klabu ya Queens Park Rangers Anton Ferdinand, ambaye alimshutumu kumtolea matamshi ya kibaguzi wakati wa mchuano wa ligi ya kuu ya England mwezi Oktoba mwaka jana. Upande wa utetezi wa Terry ulisema mteja wake alikuwa akirudia tu maneno ya kibaguzi ambayo alishutumiwa kuyatumia dhidi ya Ferdinand wakati wa majibizano ya uwanjani ambayo yalianza kutokana na madai ya utata ya mkwaju wa penalti. Terry mwenye umri wa miaka 31 huenda akatozwa faini ya hadi pauni 2,500 ikiwa atakuwa mwanasoka wa kwanza mkuu kutoka Uingereza kupatikana na hatia ya ubaguzi wa rangi katika mchuano.

Ferdinand ambaye ni mweusi alitoa ushahidi wake kuwa awali hakumsikia Terry akitumia lugha ya kibaguzi wakati wa mchuano huo. Alisema alijua tu kwamba Terry alimtolea matamshi ya kibaguzi wakati mkanda wa video ulipoonyeshwa kwenye mtandao wa youtube. Anasema angeripoti kisa hicho kwa polisi ikiwa angesikia kile kilichosemwa na Terry wakati wa mchuano huo.

Matayarisho ya kabla ya msimu

Timu mbalimbali zinaendelea kujitayarisha tayari kwa msimu mpya wa ligi za kitaifa kote barani Ulaya. Ni wakati ambapo timu zinafanya ziara katika nchi mbalimbali na kucheza mechi za kijinoa makali huku pia wakufunzi wakilenga kuimarisha vikosi vyao kwa kuwasajili wachezaji wapya. Katika ligi ya hapa Ujerumni Bundesliga, klabu ya Bayer Leverkusen imemsajili mshambuliaji wa Chile Junior Fernandes kwa mkataba wa miaka mitano kutoka klabu ya Universidad de Chile.

Andrea Pirlo ni kiungo wa kutegemewa katika klabu ya Juventus ya Italia
Andrea Pirlo ni kiungo wa kutegemewa katika klabu ya Juventus ya ItaliaPicha: AP

Leverkusen ilitangaza usajili wa mchezaji  huyo mwenye umri wa miaka 24 Ijumaa na ikasema vilabu vyote viwili vilikubaliana kutofichua kiasi cha fedha walichotumia. Leverkusen imesema Fernandes atajaza pengo lililoachwa na mshambuliaji wa Switzerland Eren Derdiyok aliyehamia klabu ya Hoffenheim. Mkurugenzi wa Spoti Rudi Voeller amesema Fernandes ana uwezo wa kiufundi na kimwili, pamoja na kasi mbele ya lango.

Klabu ya Bayern Munich leo imepuuzilia mbali uvumi kuwa inalenga kumsajili kiungo wa Italia Andrea Pirlo kutoka klabu ya Juventus. Kulingana na ripoti za magazeti ya Italia, ni klabu hiyo ya Bundesliga imetoa ombi la euro milioni 10 kuipata sahihi ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 ambaye ana mkataba na Juve hadi mwaka wa 2014.

Mwenyekiti wa Bayern Karl-Heinz Rummenigge amesema katika taarifa kuwa klabu hiyo haijatoa ombi lolote kwa Juventus wala kuwasiliana na mchezaji huyo pamoja na washauri wake. Pirlo alionyesha umahiri wake katika fainali za UEFA EURO 2012 zilizokamilika hivi majuzi wakati Italia iliishinda Uingereza kwa penalti na kufuzu katika nusu fainali kabla ya kuzabwa na Uhispania magoli manne kwa sifuri katika fainali.

Katika habari nyingine za Bundesliga ni kuwa Kiungo Andreas Ottl ameondoka katika klabu iliyoshushwa daraja ya Hertha Berlin na kujiunga na klabu ya Augsburg kwa mkataba wa miaka miwili. Ottl mwenye umri wa miaka 27 mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani kwa wachezaji wa chini ya umri wa miaka 21, na akacheza mechi 135 akiwa na vilabu vya Bayern Munich, Nuremberg na Hertha.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef