1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson: Makubaliano ya COP26 ni ya kihistoria

15 Novemba 2021

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameyasifu makubaliano ya mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi uliomalizika mjini Glasgow akisema yanafungua njia ya "mageuzi makubwa".

https://p.dw.com/p/42zS0
COP26 in Glasgow
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson Picha: Alberto Pezzali/picture alliance/AP

Johnson aliyekuwa mwenyeji wa mkutano huo wa COP26 huko Sotland amesema makubaliano yaliyopatikana kwa taabu mjini Glasgow ni ya kihistoria na yanachora ramani ya jinsi mataifa yatakabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani.

Kiongozi huyo alikuwa akizungumza kwenyemkutano na waandishi habari wa kutoa tathmini ya mkutano wa COP26 uliomalizika mwishoni mwa juma baada ya wiki mbili nzito za majadaliano miongoni mwa wawakilishi wa mataifa duniani.

Johnson amesema moja ya mafanikio makubwa ya mkataba uliopatikana ni shinikizo kwa ulimwengu kuachana na matumizi ya nishati ya makaa ya mawe inayohusishwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira.

Amesema ahadi ya bara la Ulaya na Marekani ya kuondoa ufadhili kwenye miradi ya makaa ya mawe na mafuta mazito ni hatua muhimu kuelekea usitishaji matumizi ya nishati chafuzi.

"Lakini pamoja na tofauti zetu zote, bila shaka ulimwengu unaelekea kwenye njia sahihi. Hata kwa yule mwenye mashaka makubwa zaidi atakwambia kwamba lile lengo la kuzuia kupanda kwa joto duniani kwa nyuzi 1.5 bado liko hai" amesema Johnson.

Johnson asema safari lakini bado ni ndefu

Titel: UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow
Picha: Jeff J. Mitchell/Getty Images

Hata hivyo licha ya mafanikio aliyoyataja,  Johnson pia amekiri kuwa mkutano huo wa COP26 haukutoa suluhisho kamili la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani.

Ametolea mfano ilivyokuwa vigumu kuyalazimisha mataifa yote kukomesha matumizi ya makaa ya mawe akizitaja China na India kuwa zilidhoofisha lugha iliyotumika kwenyemakubaliano ya mwisho baada ya nchi hizo mbili kusema zinahitaji muda zaidi kabla ya kuachana na nishati ya makaa ya mawe.

Johnson amesema bila shaka madola hayo mawili yatafaa kujieleza juu ya kwanini yanajivuta vuta kuchukua hatua katika wakati baadhi ya mataifa yanakabiliwa na kitisho cha kupanda kwa kina cha bahari, ukame na moto wa mwituni kama sehemu ya taathira chungunzima za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuwa kitisho cha mabadiliko ya tabianchi "bado kipo mlangoni". Naye kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ameyataka mataifa yaliyo na uwezo kufanya kila liwezekanalo kuipusha dunia na zilzala ya kupanda kwa kiwango cha joto.

Mataifa masikini yasubiri msaada wa kifedha bila mafanikio 

UN-Klimakonferenz COP26 in Glasgow
Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Makubaliano ya mjini Glasgow yanakuwa ya kwanza baada ya miaka 25 ya majadiliano ya aina hiyo kwa nishati za makaa ya mawe na mafuta-- zinazotajwa kuwa chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabianchi-- kuorodheshwa kwenye nakala ya mwisho ya mkataba.

Hata hivyo kizungumkuti bado kimesalia kwa mataifa masikini yaliyo na dhima ndogo kwenye suala la mabadiliko ya tabianchi.

Wawakilishi wa mataifa hayo walitumia wiki mbili mjini Glasgow kudai msaada mahsusi wa kifedha kuyawezesha kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Lakini kwa bahati mbaya wawakilishi wa madola tajiri walikusanya virago huko Scotland bila kutoa ahadi yoyote ya maana kuhusu fedha zilizoombwa.

Pengine matarajio itakuwa kwenye mkutano wa COP27 utakaofanyika nchini Misri mwaka unaokuja.