1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jopo la UN laanza kutoa uamuzi wa kesi ya mauaji ya Hariri

18 Agosti 2020

Majaji wa mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kuhusu Lebanon, wamesema kuna ushahidi wa kutosha kuwahusisha wanachama wawili wa kundi la Hezbollah katika mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu Rafik Hariri

https://p.dw.com/p/3h8qE
Libanon Beirut | Rafik Hariri | Proteste
Picha: picture-alliance/dpa/T.Kluiters

Akifafanua mazingira ya kisiasa yaliyotangulia mauaji ya waziri mkuu Hariri, Jaji anayeongoza mahakama hiyo maalum kwa Lebanon  David Re, alisema kuwa miezi kadhaa kabla ya kifo chake, Hariri alikuwa anaunga mkono kupunguzwa kwa ushawishi wa Syria na kundi la Hezbollah nchini Lebanon. Alisema kuwa majaji waliochunguza ushahidi uliosalia katika kesi dhidi ya wanachama wanne wa kundi la Hezbollah wanaotuhumiwa kwa kuhusika katika ulipuaji huo wa bomu walikuwa na mtazamo kwamba Syria na Kundi laHezbollah zilikuwa na nia ya kumuuwa Hariri na baadhi ya washirika wake wa kisiasa.

Hata hivyo majaji hao walisema hakuna ushahidi wa kuihusisha moja kwa moja Syria iliyokuwa na mwingilio mkubwa wa kijeshi katika nchi hiyo ama uongozi wa kundi la Hezbollah katika shambulizi hilo. Uamuzi wa mwisho utatolewa baadaye leo katika mahakama hiyo nje ya mji wa The Hague nchini Uholanzi ambapo watu wengine wanne wanaodaiwa kuwa wanachama wa kundi la Hezbolla wanashtakiwa bila kuwepo.

Sayyed Hassan Nasrallah Hisbollah-Chef
Mkuu wa kundi la Hezbollah- Hassan NasrallahPicha: picture-alliance/dpa/N. Mounzer

Mahakama hiyo imesema kuwa kesi dhidi yao inasilikizwa katika misingi ya ushahidi usiokuwa wa moja kwa moja. Uamuzi huo unatarajiwa kuchukuwa saa kadhaa huku hukumu hiyo ikijumuisha zaidi ya kurasa 2600.

Hata hivyo rais wa Lebanon Michel Aoun amesema kuwa uamuzi unaotarajiwa kutoka kwa mahakama hiyo umechelewa kuleta haki kamili. Katika mahojiano na gazeti la Corriere della sera la  Italia, Aoun amesema kuwa anasubiri uamuzi huo na kwamba atauheshimu. Aliongeza kuwa hataki kusema zaidi mbali na kwamba miaka 15 imepita tangu tukio hilo la mauaji na kwamba haki baada ya muda mrefu kama huo sio haki tena.

Jaji David Re aliitaka mahakama hiyo izingatie dakika moja ya ukimya kuwakumbuka waathiriwa wa tukio hilo, wale waliofariki, waliojeruhiwa, familia zao na wale waliopoteza makazi. Mwanamwe Hariri wa kiume Saad ambaye pia aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu pia alikuwepo katika mahakama hiyo iliyokuwa na ulinzi mkali kusikiliza uamuzi wa jopo hilo.

Mkuu wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah alikataa kuwasalimisha washukiwa hao wanne na kupinga uhalali wa mahakama hiyo.Jopo hilo maalum kwa Lebanon iliundwa mnamo mwaka 2007 na limekuwa likiwasomea mashtaka wanne hao bila uwepo wao katika muda wa miaka sita iliyopita.