Joto la Uchaguzi Mkuu lapanda nchini Tanzania
8 Julai 2020Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii katika serikali iliyopita aliyehamia CHADEMA, Lazaro Nyarandu ni miongoni mwa makada wa chama hicho ambao leo wamejitokeza kwenye ofisi za chama akichukua fomu hatua inayomfanya sasa aungene na mwanasiasa mwenzake, Tundu Lissu katika mbio hizo za kuwania urais ndani ya chama.
Wanasiasa wote hao wawili ambao wamejitokeza kuchukua fomu wanatajwa kuwa na ushawishi mkubwa kwa wapiga kura ingawa mmoja wake anasemekana kuwa na ushawishi mkubwa zaidi ndani na nje ya chama.
Jumla ya wagombea 11 awali walitangaza nia zao kutaka kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa mwezi Oktoba, hatua ambayo imeshuhudiwa kwa mara ya kwanza kwa chama hicho kuwa na idadi kubwa ya wagombea tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma, kulikoshuhudiwa jina moja au mawili tu yaliyokuwa yakijitokeza.
Swali kubwa linalojitokeza sasa ni kwa kiasi gani chama hicho kitafanikiwa kuvuka salama kwenye mchakato huo wa kumpata mgombea mmoja na hatimaye kuungwa mkono na wanachama wote.
Nafasi za ubunge nako moto ni mkali
Wakati hayo yakiwa kwenye ungwe ya urais, wakati huu pia kunashuhudiwa idadi kubwa ya wanasiasa wanaoendelea kujitokeza wakitangaza nia zao za kutaka kuwania nafasia za ubunge katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Chama tawala CCM ndicho kinachoonekana kuongoza kwa kuwa na makada wengi wanaojitokeza hadharani ambao wameyabainisha maeneo wanayokusudia kuongeza ushawishi wao kwa ajili ya kusaka kura.
Majimbo yaliyoko eneo la kaskazini kama vile Kilimanjaro na Arusha maeneo ambayo ni ngome ya chadema yanatarajiwa kuwa na ushindani mkali zaidi hasa kutokana na kuwavutia wanasiasa wengi ambao wameonyesha nia zao.
Hali hiyo inafanya mtihani wa kubashiri kama majimbo hayo yataendelea kubakia mikoni mwa upinzani ama kwenda CCM kuwa ngumu hasa kutokana na mwenendo mpya wa kisiasa unaoendelea kushuhudiwa sasa.
Wakati hayo yakiendelea hivyo, baadhi ya wateule wa rais kama vile wakuu wa mikoa na wilaya waliokuwa na kiu ya kutaka kuwania ubunge sasa wameanza kujiweka kando wakisitisha mipango yao,baada ya onyo la mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ambaye awali alikuwa na mipango ya kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini, ni miongoni mwa wale waliyoyaweka kabatini mawazo yao kwa sasa.
Hata hivyo, duru za habari zinasema kuwa baadhi ya wateule hao bado wanaendelea kupima upepo kuangalia kama wajitose kwenye mbio za ubunge au kusitisha moja kwa moja mipango yao.