Joto la uchaguzi mkuu Nigeria lapanda
19 Desemba 2006Rais Olusegun Obasanjo, huenda ana matumaini ya kuwa kwa kumpigia upatu, mwanasiasa asiye maarufu, Umaru Yar Adua kama mrithi wake wa kiti hicho, kutampa nafasi ya kutoshtakiwa na pia kuwa na nguvu na serikali itakayokuwa madarakani baada ya kung’atuka mwezi ujayo.
Lakini wadadisi na wale wanaomfahamu Umaru Yar Adua ambaye ni gavana wa jimbo la Katsina, wanasema kuwa mwanasiasa huyo hatokuwa tayari kuongozwa na Obasanjo iwapo atashinda katika uchaguzi wa mwezi April.
Wiki iliyopita Umaru alichaguliwa na chama tawala , kuwania nafasi hiyo ya urais wa nchi hiyo ya afrika magharibi.
Kufuatia mabadiliko yaliyofanywa ndani ya chama tawala cha Peoples Democratic Party PDP Obasanjo atabaki kuwa mwenyekiti wa chama hicho na hivyo kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama.
Wakati huo huo chama cha upinzani All Nigeria Peoples OParty nacho kimemteuwa Kiongozi wa zamani wa kijeshi Muhammad Buhari kuwa mgombea wake, baada ya wagombea sita wengine kujiondoa.
Meja Jenerali mstaafu Buhari aligombea uchaguzi wa Rais 2003 na kushindwa na Obasanjo. Buhari anaafahamika kuwa ni mtu wa vitendo, akikumbukwa wakati wa utawala wake 1983 baada ya kuipindua serikali ya kiraia ya Alhaji shehu Shagari.
Buhari alijaribu kupambana na rushwa , lakini katika kile wadadisi wanachokiita kwenda haraka mno, hatimae aliangushwa na wanajeshi wenzake Agosti 1985 na hatamu uongozi kushikwa na Jenerali Ibrahim Badamasi Babangida maarufu –IBB.
Babangiada alijiondoa wiki iliopita katika kinyanganyiro cha kugombea kwa tiketi ya PDP, katika kile kilichoonekana kuwa ni kujiepusha na izara , baada ya kufahamika kwamba Obasanjo akimpigia debe Yáradua.
Jee kutokeaza kwa watu hawa wawili Yaradua na Buhari kunatoa changa moto gani kwa uchaguzi ujao nchini humo na je hatua hii imepokewaje na Wanigeria ambao kwa sehemu fulani wamegawika kieneo, kati ya Wahausa, Wayoruba na waibo ?
Uchaguzi wa ujao nchini Nigeria, taifa la wakaazi wengi kabisa barani Afrika utafanyika Aprili Mwakani.Kwa mujibu wa takwimu za mwaka jana Nigeria ina wakaazi kiasi cha millioni 130.