Juhudi za kuimarisha biashara baina ya mataifa ya kusini .
1 Juni 2004Kundi la nchi 44 zinazoendelea limeamua kuufufua mkataba wao wa zamani wenye lengo la kukuza biashara miongoni mwa mataifa ya kusini na kuanza mazungumzo mapya ya biashara. Hayo yana lengo la kufungamana na mueleke mpya wa uchumi na biashara duniani. Hatua hiyo itatoa msukumo zaidi katika utaratibu ulipo wa biashara baina ya nchi za kusini na kusini- alitamka hayo Luiz Felipe de Seixas Correa- Balozi wa Brazil katika taasisi za kimataifa zenye makao makuu mjini Geneva.Mbrazil Rubens Ricupero Katibu mkuu wa Shirika la biashara na maendeleo la Umoja wa mataifa (UNCTAD) naye akasema moja wapo ya alama muhimu za wakati huu katika safu ya biashara duniani ni ukuaji imara wa biashara miongoni mwa nchi zinazoendelea.´
Makubaliano hayo kati ya nchi zinazounda kundi la mataifa 44 yanayoendelea ulianzishwa kufuatia mazungumzo magumu katika miaka ya 1980 baina ya kundi la mataifa sabini na saba-G 77, likiwa ni kundi la nchi zinazoendelea.Hivi sasa kundi hilo lina jumla ya nchi 135 wanachama- ukiwa ni muungano mkubwa kabisa ndani ya umoja wa mataifa. Jina lake linatokana na idadi ya wanachama wa awali wakati lilipoundwa 1964 hatua iliotokea sambamba na kuundwa kwa shirika la biashara na maendeleo la umoja wa mataifa UNCTAD.Sherehe ya miaka 40 ya kundi la 77 zitafanyika mjini sao Paulo Brazil wakati wa kikao cha UNCTAD kuanzia tarehe 13 hadi 18 ya mwezi huu wa Juni.Katika kipindi hicho, mawaziri wa biashara watakua na mazungumzo kuhusu awamu ya tatu ya makubaliano ya kimataifa juu ya utaratibu wa nafuu za kibiashara miongoni mwa nchi zinazoendelea unaojulikana kwa ufupi kama GSTP –hatua ambayo itaanza Novemba na kudumu muda wa miaka miwil.
Mpango wa GSTP ni kuzialika nchi za kundi la 77 kujiunga na makubaliano hayo, kukitolewa mualiko maalum kwa Jamhuri ya umma wa China.Katibu mkuu wa shirika la UNCTAD anasema ukuaji uchumi wa China ni moja wapo ya mambo yalioshajiisha haja ya kutanuliwa biashara kati ya nchi za kusini .Akaongeza kwamba uzito wa China katika biashara miongoni mwa ulimwengu unaoendelea ni muhimu, lakini akakumbusha kwamba India na mataifa mengine ya Asia yana ushawishi mkubwa pia yakiongeza biashara zao katika soko la dunia.Mkataba ama makubaliano ya kwanza ya utaratibu huo wa kimataifa wa nafuu za biashara ulisainiwa Thailand 1988 na kuanza kufanya kazi mwaka uliofuata baada ya kuidhinishwa na nchi 40.
Nafuu hizo za biashara zinahusika na bidhaa zipatazo 1,826,Kwa mujibu wa duru zinazohusika, utaratibu mpya utakaonza Novemba, utakua na sheria tafauti. Wale watakaotaka kupatiwa nafuu za biashara kuhusika na bidhaa zao, watabidi nao kulipia kwa kutoa nafuu fulani upande wao .Wadadisi wanasema uamuzi wa kuuzindua upya mkataba huo, unafungua njia ya kuwepo majadiliano zaidi miongoni mwa nchi zinazoendelea katika Shirika la biashara na maendeleo UNCTAD.Hapana shaka mkutano wa shirika hilo mjini Sao Paulo baadae mwezi huu, utakua ni nafasi ya kudhibitisha azma hiyo ya nchi zinazoendelea na mambo hayatotendeka kwa masharti ya nadharia kama ilivyokua siku za nyuma. Bali lengo litakua ni kuimarisha biashara kati ya kusini na kusini na kufungua njia ya majadiliano mapya.