Juhudi zaidi zinahitajika kukabiliana na Ebola
26 Septemba 2014Umoja wa Mataifa hapo jana uliitisha kikao cha dharura kujadili namna ya kukabiliana na ugonjwa huo hatari ambao kufikia sasa umewaua kiasi ya watu 3,000.
Rais wa Marekani Barrack Obama ameonya kuna mapengo makubwa kati ya misaada inayotolewa na kile kinachohitajika hasa kupambana na janga hilo la kiafya.
Viongozi wa nchi za magharibi mwa Afrika zilizothiriwa vibaya na Ebola pia wametoa wito wa kuongezwa kwa misaada huku rais wa Sierra Leone Ernest Bai Komora akilitaja janga la Ebola kuwa baya zaidi ya ugaidi.
Benki ya dunia yatoa msaada zaidi
Rais wa benki ya dunia Jim Yong Kim alitangaza katika mkutano huo kuwa benki hiyo itatoa msaada wa dola milioni 400 zaidi kusaidia kukabiliana na Ebola nchini Guinea,Liberia na Sierra Leone.
Naye rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso ametangaza umoja huo utaongeza kiasi kingine cha dola milioni 40 kupambana na Ebola.
Lakini licha ya nchi kadhaa na asasi za kimataifa kuahidi kutoa misaada,bado janga hilo linazidi kunoa makucha. Wataalamu wa afya wameonya juhudi zinazoshuhudiwa kufikia sasa hazitoshi kupambana na janga hilo kwani raslimali zaidi zinahitaji haraka mno katika nchi zilizoathirika.
Taasisi ya Marekani ya kudhibiti na kuzuia magonjwa CDC mapema wiki hii ilionya kuwa idadi ya watakaoathirika na Ebola itapanda maradufu na kufikia watu zaidi ya milioni moja na laki nne ifikapo mwezi Januari mwakani iwapo juhudi za kimataifa hazitaimarishwa.
Ebola yaathiri uchumi na kutishia uthabiti
Juu ya kusababisha vifo na kuzua hofu,Ebola imeathiri uchumi wa nchi za magharibi kutokana na baadhi ya hatua kali zinazochukuliwa na nchi kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.
Utafiti uliotolewa na benki ya dunia umebaini mfumko wa bei wa bidhaa za kimsingi licha ya juhudi za serikali kujaribu kudhibiti, bei za bidhaa ziko juu mno kutokana na uhaba na watu kununua zaidi ya mahitaji yao ya kawaida kuhofia msukosuko wa masoko.
Mbali na hayo wachambuzi wa masuala ya kiusalama wanaonya huenda Ebola ikachochea pia mizozo ya kisiasa katika nchi zilizoathirika na kusambaratisha juhudi za muda mrefu za kurejesha uthabiti katika kanda hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Rais Obama hii leo ataongoza mkutano unaozileta pamoja nchi 44 ambazo zimejiunga na ajenda yake ya kimataifa kuhusu usalama wa afya kutafuta mikakati zaidi ya kukabiliana na Ebola.
Mwandishi:Caro Robi/Ips/Ap
Mhariri:Gakuba Daniel