Jumla waliokufa kwa joto hija imepindukia watu 1,000
23 Juni 2024Hija ni moja ya nguzo tano za Uislamu ambazo Waislamu wote wenye uwezo lazima wakamilishe angalau mara moja maishani mwao.
Wanadiplomasia kutoka nchi za Kiarabu wameliambia shirika la Habari la AFP mapema wiki hii kwamba raia wa Misri 658 waliokufa wakati wa kuhiji, 630 walikwenda Makka lakini hawakusajiliwa. Rais Abdel Fattah El-Sisi amemwamuru Waziri wake mkuu Moustafa Madbouly kuchunguza kiini cha mkasa huo.
Waziri huyo Mkuu wa Misri ameamuru kampuni 16 za utalii zinyang'anywe leseni zao na mameneja wake wafikishwe kwa mwendesha mashtaka wa umma kujibu mashataka ya kuwapeleka mahujaji kwa njia haramu katika mji mtakatifu wa Makka.
Baraza la mawaziri linataka faini zitakazotozwa wahusika wa mkasa huo zipewe familia za mahujaji waliokufa. Taarifa ya baraza la mawaziri iimesema kwamba idadi kubwa ya vifo vya mahujaji wa Misri ambao hawakusajiliwa imetokana na baadhi ya makampuni ambayo yaliandaa programu za Hijja kwa kutumia viza ya ziara za kibinafsi, ambazo zinazuia wamiliki wake kuingia katika mji wa Makka.