1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya ECOWAS na juhudi za kidiplomasia nchini Mali

Saleh Mwanamilongo
17 Julai 2020

Ujumbe wa Jumuiya ya Uchumi wa mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS unafanya mazungumzo na pande husika katika mzozo wa Mali ilikutafuta suluhisho la kudumu.

https://p.dw.com/p/3fVZY
Wafuasi wa vuguvugu la M5 wakiandamana mjini Bamako.
Wafuasi wa vuguvugu la M5 wakiandamana mjini Bamako.Picha: Reuters/M. Rosier

Ujumbe wa Jumuiya ya Uchumi wa mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS unafanya mazungumzo na pande husika katika mzozo wa Mali ili kujaribu kutuliza maandamano ya kutaka kujiuzulu kwa rais wa nchi hiyo. Ujumbe huo unaoongozwa na rais wa zamani wa Nigeria, Goodluck Jonathan unatarajiwa kukutana baadae leo na rais Ibrahim Keita.

Miongoni mwa wajumbe hao wa ECOWAS ni pamoja na wanasiasa na wataalamu wa masuala ya katiba, ambao wanajaribu kuwapatanisha viongozi wa waandamanaji na serikali ya Mali. Baada ya kutofikiwa kwa maelewano katika kikao cha kwanza baina ya pande hizo mbili, vuguvugu la waandamanaji la M5 linamtaka Rais Ibrahim Boubacar Keita ajiuzulu. Issa Kaou Djim, msemaji wa waandamanaji anasema ujumbe wa ECOWAS unataka kuinusuru serikali ya Rais Keita.

''Eti leo tunatakiwa kufunga macho baada ya Rais Keita na waziri mkuu wake kuwaua watu 23, ili kuzungumzia mageuzi nchini. Tunasikitishwa kuona kwamba ujumbe wa ECOWAS haujazingatia swali muhimu. Ni wazi kwamba tatizo limefahamika, raia wanajuwa tatizo liko wapi, tatizo ni Rais Keita ambao raia hawataki tena uongozi wake''alisema Djim.

Hata hivyo, vuguvugu hilo la upinzani na asasi za kiraia nchini Mali, lilitoa mwito wa kuahirishwa kwa maandamano yaliyopangwa hii leo Ijumaa kwa hofu ya machafuko zaidi nchini humo. Lakini uliandaa ibada kwa ajili ya waandamanaji waliouawa. Waziri Mkuu wa Mali, Boubou Cisse anasema kwamba serikali yake inaunga mkono juhudi za ECOWAS katika kutafuta suluhisho la mzozo huo.

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita.
Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

''Nia ya Rais Keita ni yangu mimi kama waziri mkuu, nia ya ujumbe huu wa ECOWAS ni kwamba taratibu hii ya kisiasa itupeleke hadi kwenye suluhisho la kudumu la mzozo, kwa maslahi ya jumla ya wananchi wa Mali''.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Cisse, machafuko ya mwishoni mwa wiki iliyopita yalisababisha vifo vya watu 11. Umoja wa Mataifa ulielezea kwamba watu 14 waliuawa, huku vuguvugu la M5 likisema kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha ni 23.

Waziri Mkuu Cisse anasema kwamba uchunguzi unaendeshwa na wahusika watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Upinzani unaelezea kwamba Rais Keita ndie anayewajibika kuhusu machafuko hayo.

Katika juhudi za kumaliza maandamano nchini mwake, Rais Keita alitangaza kuunda serikali ya mseto na kuivunja mahakama ya kikatiba, ambayo uamuzi wake wa kubatilisha matokeo ya awali ya uchaguzi wa bunge mapema mwaka huu, ulikuwa kiini cha maandamano hayo. Licha ya tangazo hilo la Rais Keita, viongozi wa waandamanaji wanaendelea kumtaka ajiuzulu.