Kabul: Vikosi vya Marekani vyawekwa kwenye tahadhari kubwa
28 Agosti 2021Raia wote wa Marekani walitakiwa waondoke kwenye lango la Abbey kwenye uwanja huo wa ndege, na pia upande wa Mashariki na Kaskazini mwa uwanja wa Hamid Karzai mjini Kabul. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani pia ilisisitiza ushauri wake kwa raia wake wa kuepuka kuufikia uwanja huo wa ndege.
Taliban wamepeleka vikosi vya ziada karibu na uwanja huo wa ndege wa Kabul kuzuia umati mkubwa wa watu wanaokusanyika katika eneo hilo tangu wiki mbili zilizopita kwa lengo la kutaka kundoka Afghanistan.
Hatua hiyo imechukuliwa siku mbili baada ya kutokea shambulio kubwa la kujitoa muhanga mjini Kabul wakati ambapo Marekani inaendelea na shughuli za kuwaondoa raia wake na wale wa Afghqnistan kutoka nchini humo kabla ya tarehe ya mwisho ambayo ni Agosti 31.
Mataifa mengi ya Magharibi tayari yamekamilisha zoezi la kuwahamisha watu kutoka Afghanistan kabla ya tarehe hiyo ya mwisho ambayo ni siku ya Jumanne siku inayotarajiwa kuwa Marekani itakuwa imeviondoa vikosi vyake vyote kutoka nchini humo.
Shambulio la kujitoa mhanga lilifanywa mnamo siku ya Alhamisi na mpiganaji wa kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiisilamu IS. Miongoni mwa watu waliouawa ni Waafghanistan 169 na wanajeshi 13 wa Marekani. Pana wasiwasi mkubwa kwamba kundi hilo ambalo lina itikadi kali zaidi kuliko la Taliban huenda likafanya mashambulizi mengine.
Jeshi la Marekani limemuua mtu anayedaiwa kupanga shambulizi hilo la kwenye uwanja wa ndege wa Kabul kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuahidi kwamba nchi yake ingelipiza kisasi.
Zaidi ya watu 110,000 wameshahamishwa kupitia uwanja wa ndege wa Kabul tanguTaliban ilipochukua udhibiti wa nchi ya Afghanistan, kulingana na Marekani, ikiwa ni pamoja na karibu watu 6,800 waliohamishwa katika muda wa saa 24 zilizopita. Maelfu zaidi wanajitahidi kuipata nafasi ya kuondoka lakini huenda wasifanikiwe kufikia hiyo Jumanne.
Wakati huo huo shirika la chakula la Umoja wa Mataifa limetoa tahadhari kuwa ukame unazidi kutishia maisha ya watu zaidi ya milioni 7. Shirika hilo la Chakula na Kilimo FAO limesema Waafghanistan pia wanateseka kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya corona na wengi wao hawana makazi kutokana na mapigano ya hivi karibuni.
Mapema mwezi huu, Shirika hilo la Mpango wa Chakula Ulimwenguni la Umoja wa Mataifa lilikadiria kuwa takriban mtu mmoja kati ya watu watatu nchini Afghanistan yenye watu wapatao milioni 14 anahitaji msaada wa chakula haraka.
Vyanzo:/DPA/AP