Kabul: Zaidi ya watu 30 wauawa kwenye mlipuko wa bomu
9 Mei 2021Haikufahamika mara moja kilichosababisha mlipuko huo. Kulikuwa na taarifa zinazopingana juu ya kilichosababisha mlipuko. Awali baadhi ya vyombo vya habari vya viliripoti juu ya kutokea milipuko mitatu iliyosababishwa na roketi, wakati ripoti zingine zilidokeza kuwa mlipuko huo ulisababishwa na bomu lililolipuka kutoka kwenye gari.
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani amewalaumu wapiganaji wa kundi la Taliban kwa mashambulio hayo, amesema kundi hilo linaonyesha kuwa halina nia ya kuutatua mgogoro wa nchi hiyo kwa amani na hivyo linauhujumu mchakato wa amani, hayo ni kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.
Hata hivyo Taliban imekana kuhusika na mashambulio hayo pia imelaani mauaji hayo yaliyowalenga raia.
Soma Zaidi:Blinken aahidi uungaji mkono wa Marekani kwa Afghanistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani Tariq Arian amesema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka baada ya mashambulio hayo ya bomu yaliyotokea katika kitongoji cha Dasht-e-Barchi kwenye eneo la shule ya Syed Al-Shahda na kwamba watu wapatao 55 waliojeruhiwa wamepelekwa kwenye hospitali mbalimbali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Shirika la Uingereza linaloshughulikia hali za dharura na ambalo linaendesha kituo matibabu mjini Kabul limesema limepokea watu 26 waliojeruhiwa kwenye mlipuko huo.
Taarifa zaidi zinafahamisha kwamba mlipuko huo wa bomu ulitokea wakati wakaazi wengi walipokuwa wakifanya manunuzi katika maandalizi ya kuelekea sikukuu ya Eid-al-Fitr. Eneo hilo linalokaliwa kwa kiasi kikubwa na jamii ya washia wa Hazara limekuwa likilengwa na wanamgambo wa Kisunni.
Juhudi za kutafuta amani kati ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban ili kumaliza vita vya miongo kadhaa zimekuwa zikilegalega.
Shambulio hilo la bomu linaongeza hofu kwamba vurugu katika nchi ya Afghanistan iliyokumbwa na vita zinaweza kuongezeka wakati ambapo Marekani na jumuiya ya kijeshi ya NATO zinaazimia kuyaondoa majeshi yao baada ya kuwemo nchini humo kwa karibu miaka 20.
Soma Zaidi:Nchi za NATO zakubaliana kuondoka Afghanistan
Tangu tarehe mosi Mei, wanajeshi wa kimataifa walianza rasmi kuondoka kutoka nchini Afghanistan na mchakato huo unapaswa kukamilika ifikapo Septemba 11 mwaka huu au mapema.
Balozi wa Marekani nchini Afghanistan Ross Wilson amesema kwenye Twitter kwamba shambulio hilo ni kitu cha kuchukiza na ni unyama dhidi ya binadamu wasio na hatia.
Vyanzo: DPA/AFP/AP