1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kabwe: Serikali iombe msamaha kuhusu vifo vya ajali ya ndege

24 Novemba 2022

Mwanasiasa wa upinzani Tanzania Zitto Zuberi Kabwe, ameitaka serikali kuwajibika, au kuomba msamaha kwa Watanzania kutokana na uzembe uliofanyika wakati wa ajali ya ndege iliyotokea Novemba sita.

https://p.dw.com/p/4K0Kj
Tansania | Flugzeugabsturz in den Victoriasee
Picha: SITIDE PROTASE/AFP

Siku moja baada ya kuvuja kwa ripoti ya awali ya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision Air,  nchini Tanzania, Kiongozi Mkuu wa Chama cha Upinzani, ACT Wazalendo, ZittoZuberi Kabwe, ameitaka serikali kuwajibika, au kuomba msamaha kwa watanzania kutokana na uzembe uliofanyika wakati wa ajali hiyo iliyotokea Novemba sita. 

Ripoti hiyo ambayo msemaji wa serikali ya Tanzania aliikanusha baada ya kunukuliwa na vyombo vya habari vya ndani na kimataifa, ilibaini kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe na kwamba endapo jitihada zingefanyika, huenda vifo visingetokea.

Soma pia: Tanzania kuaga miili ya waliofariki katika ajali ya ndege

Sasa kiongozi Mkuu wa Chama cha Upinzani Tanzania, ACT Wazalendo Zitto Kabwe, katika mkutano wake na waandishi wa habari amesema wizara husika zilitakiwa kuomba radhi na kuwajibika.

Zitto Kabwe asema wizara husika zilitakiwa kuomba radhi na kuwajibika kufuatia vifo vilivyotokea.
Zitto Kabwe asema wizara husika zilitakiwa kuomba radhi na kuwajibika kufuatia vifo vilivyotokea.Picha: DW/S. Khamis

"Nilitarajia waziri wa mambo ya ndani, na uchukuzi kuomba msamaha na kuwajibika. Angalau kukubali kuwa kulikuwa na uzembe na kuomba radhi,” amesema Kabwe.

Zitto ameyasema hayo, ikiwa ni siku 18 baada ya ajali ya ndege ya Precision Air, iliyoanguka katika Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19, na kuogeza kuwa ripoti iliyosambaa Jumatano ya Wizara ya Uchukuzi ni ya serikali na hivyo kuitaka serikali iache kuikana ripoti hiyo na endapo itabainika kuwa ripoti hiyo si ya serikai, basi yupo tayari apelekwe mahakamani.

Msigwa ashikilia kuwa ripoti rasmi ya uchunguzi haijatolewa

Hata hivyo, mkurugenzi wa habari na Mawasiliano, Gerson Msigwa alipopigiwa simu kuzungumzia kile alichokisema Zitto Kabwe, ameshikilia msimamo wake alioutoa Jumatano kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii.

”Lakini tumeshasema iwe alichosema ni sahihi au si sahihi ile taarifa haijatoka serikali, sisi serikali ndo ingetoa,” amesema Msigwa.

Wavuvi waliofika eneo la mkasa baada ya takribani dakika tano, walisaidia katika juhudi za uokozi na kuwatoa manusurika ziwani wakitumia mitumbwi yao.
Wavuvi waliofika eneo la mkasa baada ya takribani dakika tano, walisaidia katika juhudi za uokozi na kuwatoa manusurika ziwani wakitumia mitumbwi yao.Picha: AYO TV/AP/picture alliance

Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha mhudumu wa ndege kwa kushirikiana na abiria ndio walifungua mlango na kuwezesha kuokolewa kwa watu 24. Wavuvi walifika baada ya takribani dakika tano, na waliwachukua walionusurika kwenye mitumbwi yao.

Ajali hiyo ilitokea Jumapili ya Novemba 6, 2022 ambapo ndege hiyo ilikuwa na watu 43 kati yao, 39 walikuwa abiria, marubani wawili na wahudumu wawili. 19 walifariki dunia na 24 kuokolewa.

Kulingana na ripoti hiyo, askari wenye boti 400 HP inayotumika kwa shughuli za doria na uokozi, walishindwa kuitumia wakati huo kwa kuwa haikuwa bandarini.

Je, serikali ya Tanzania ilizembea uokoaji ajali ya ndege?

Mwandishi: Florence Majani