Karibu watu 150 wafariki Libya kutokana na mafuriko
11 Septemba 2023Taarifa hii imetolewa na msemaji wa serikali ya Libya yenye makao yake kwenye mji wa Benghazi, Mohamed Massoud.
Amesema watu hao wamepoteza maisha baada ya kimbunga Daniel kuleta mvua kubwa kwenye eneo la Derna kwenye jimbo la Jabal al-Akhdar na katika viunga vya Al-Marj.
Amearifu kuwa waziri mkuu wa serikali yenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo, Oussama Hamad, mkuu wa kamati ya uokoaji ya taifa na mawaziri kadhaa wamelitembelea eneo la Derna kutathmini kiwango cha uharibifu uliotokea.
Hamad, anayeongoza serikali hasimu dhidi ya ile inayotambulika kimataifa yenye makao yake mjini Tripoli, ametangaza kuwa Derna hivi sasa ni "eneo la janga" baada ya kimbunga Daniel kulipiga eneo hilo jana Jumapili.
Vikosi vya uokoji vimepelekwa kwenye mji huo, ulioko kiasi kilometa 900 mashariki mwa mji mkuu, Tripoli.