1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi mbili za maandamano zakabiliana Ujerumani

Mohammed Khelef5 Januari 2015

Maelfu ya Wajerumani wanatarajiwa kuandamana kupinga maandamano ya kila wiki dhidi ya wahamiaji na Waislamu ambayo yamevutia waungaji mkono wengi, licha ya kukosolewa vikali na viongozi wakuu.

https://p.dw.com/p/1EFAm
Maandamano ya kupinga vuguvugu la PEGIDA mjini Dresden tarehe 22 Disemba 2014.
Maandamano ya kupinga vuguvugu la PEGIDA mjini Dresden tarehe 22 Disemba 2014.Picha: picture alliance/abaca

Waandamanaji 10,000 walitazamiwa kukusanyika kwenye mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, siku ya Jumatatu ya kwanza ya mwaka 2015 kupinga maandamano yanayopinga kusambaa kwa Uislamu nchini Ujerumani na yanayotaka kuwepo kwa sheria kali za kudhibiti wahamiaji na waomba hifadhi maarufu kama PEGIDA.

Mjini Cologne, maafisa wa mji huo walisema watazima taa zinazolimurika kanisa kuu ambalo ni kituo cha maandamano ya PEGIDA, kutokuwapa nafasi ya kufaidi muonekano wa kanisa hilo kongwe kabisa kwenye jimbo la Northrhine Westphalia na ambalo ni sehemu ya turathi za kimataifa. Waandamanaji 2,000 wanaopingana na PEGIDA, wanatazamiwa kuandamana pia.

Mjini Stuttgart kunatazamiwa kuwa waandamanaji 5,000 watamiminika mitaani jioni ya leo kupingana na kaulimbiu inayotumiwa na PEGIDA: "Wir sind das Volk", yaani "sisi ndio watu wenyewe" ambayo katika hotuba yake ya kuuaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka 2015, Kansela Angela Merkel alisema inatumiwa na waandaaji wa maandamano ya PEGIDA waliojaa chuki, dharau na bezo kwa wageni.

Chuki zasambaa mashariki

Lakini kwenye mji wa mashariki, Dresden, na ambako ndiko maandamano ya PEGIDA yalikoanzia miezi ya mwisho ya mwaka uliopita, maelfu ya waungaji mkono watajitokeza tena Jumatatu ya leo.

Profesa Werner J. Patzelt wa Chuo Kikuu cha Dresden: "Mashariki kuna hisia mbaya dhidi ya wageni kuliko magharibi."
Profesa Werner J. Patzelt wa Chuo Kikuu cha Dresden: "Mashariki kuna hisia mbaya dhidi ya wageni kuliko magharibi."Picha: picture-alliance/Eventpress Stauffenberg

Profesa Werner Patzelt wa Chuo Kikuu cha Teknolojia mjini humo, aliliambia shirika la habari la dpa kwamba vuguvugu la PEGIDA limesadifu hisia za kundi la raia ambalo linajiona kutengwa kisiasa na kiuchumi kwenye eneo hilo la mashariki. "Upande wa magharibi tayari kuna wageni na wakimbizi wengi, hivyo watu wamewazoea, lakini sio huku mashariki," alisema profesa huyo wa sayansi ya siasa.

Dresden ni mji mkuu wa jimbo la mashariki la Saxony, ambalo limekuwa likishuhudia mara kwa mara mashambulizi dhidi ya wageni yanayohusishwa na siasa za Unazi mamboleo.

Mnamo mwaka 2004, chama cha mrengo mkali wa kulia, NPD, kilipata asilimia 9.2 ya kura kwenye uchaguzi wa bunge kwenye jimbo hilo, ingawa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, chama hicho kilipata asilimia 1.3, ambayo ilikuwa chini ya asilimia 5 ambazo kingeliwezesha kuwa na kiti kwenye bunge la shirikisho, Bundestag.

Maandamano ya kupinga usilimishwaji wa Ulaya na wageni mjini Bonn, Bogida, siku ya tarehe 22 Disemba 2014.
Maandamano ya kupinga usilimishwaji wa Ulaya na wageni mjini Bonn, Bogida, siku ya tarehe 22 Disemba 2014.Picha: DW/Greta Hamann

Uungwaji mkono mkubwa kwa itikadi kali ya mrengo wa kulia miongoni mwa wakaazi wa Saxony haukifaidishi tu chama cha NPD, bali pia chama cha Alternative for Germany kinachopingana na sarafu ya euro, na hivyo pia kulipa vuguvugu la PEGIDA ngome kubwa.

Hata hivyo, utafiti wa shirika la habari la dpa unaonesha kuwa hoja kuu ya maandamano ya PEGIDA kwamba jamii ya Ujerumani inatishiwa na kugeuka kuwa ya Kiislamu ni dhaifu, kwani Waislamu ni asilimia 5 tu ya raia zaidi ya milioni 80, huku asilimia 98 ya Waislamu hao wakiishi kwenye upande wa magharibi ya Ujerumani na sio mashariki yalikoanzia maandamano ya PEGIDA, ambako kuna asilimia 0.7 tu ya Waislamu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga