Kampeni dhidi ya biashara ya kuuza watu yazinduliwa
17 Desemba 2007Shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM, limezindua kampeni ya kuumasisha umma kuhusu biashara ya uuzaji wa binadamu nchini Tanzania, nchi ambayo inazidi kutumiwa kama kituo cha usarishaji wa binadamu. Hayo ni kwa mujibu wa shirika hilo la IOM katika taarifa yake iliyotolewa mapema leo mjini Nairobi, Kenya.
Taarifa hiyo inasema visa vya uuzaji watu katika ngazi ya kimataifa na hata nchini umeongezeka nchini Tanzania, visa vingi vikifanyika ndani ya nchi. Wasichana na wavulana husarishwa kutoka mikoani na kupelekwa mijini ambako hunyanyaswa kama wafanyakazi wa nyumbani, kufanyishwa kazi ya kilimo kwa ajili ya biashara, uvuvi wa samaki na katika kampuni za kuchimba madini na ukahaba wa watoto.
Kampeni hiyo ya miezi mitatu iliyopewa jina ´Uwe Sauti Yao´ ilizinduliwa jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Dar es Salaam na utafuatiwa na matangazo katika televisheni na redio. Mabango, kalenda, fulana na makofia ni vitu vitakavyosambabzwa katika miji yote mikubwa ya Tanzania.
Kiongozi wa shirika la IOM nchini Tanzania, Par Liljert, amefurahi kwamba kampeni hiyo imeungwa mkono na waimbaji mashuhuri wa nyimbo za dini na wanamuziki wa miondoko ya hip-hop.