Kampeni Tanzania zaingia ngwe ya lala salama
9 Oktoba 2020Wagombea wa urais katika uchaguzi mkuu nchini Tanzania wanaanza kuingia ungwe ya lala salama katika kampeni zao, huku mgombea wa chama tawala CCM, Rais John Magufuli leo akirejea tena kwenye majukwaa ya kampeni baada ya kuwa na mapumziko mafupi, na mpinzani wake mkuu, Tundu Lissu wa CHADEMA, akimaliza kutumikia siku saba ya adhabu aliyopewa na Kamati ya Maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Mgombea wa CCM, Rais Magufuli, ambaye wakati huu yuko katika Uwanja wa Taifa ambao sasa unajulikana kama Uwanja wa Mkapa ulioko eneo la Temeke ametenga muda wa siku tatu kuanzia leo kuzunguka katika maeneo ya Dar es Salaam kunadi sera zake.
Akiwa anasindikizwa na kundi la wanamuziki wa kizazi kipya, mgombea huyo pamoja na kutaja yale aliyoyatekeleza katika awamu yake ya kwanza ya miaka mitano, kadhalika anatumia fursa hiyo kuwanadi wagombea wa ubunge na udiwani katika jiji ambalo lilitawaliwa zaidi na wabunge wa upinzani.
Kwa upande wa pili, mgombea wa chama kikuu cha upinzani Chadema, Tundu Lissu, anakaribia kumalizia adhabu yake yakutofanya kampeni kwa kipindi cha siku saba. Huenda akapanda tena majukwaani kuanzia kesho wakati adhabu hiyo inapokamilika leo.
Kwa kipindi chote alichokuwa akitumikia adhabu hiyo, mwanasiasa huyo amekuwa akijitambulisha upya kwa umma kwa kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye masoko makubwa na kujipatia mahitaji yake.
Leo haijafahamika atatembelea wapi, lakini hapo jana aliibukia eneo la Mlimani City na baadaye alikwenda katika soko la Manzese ambako pia alipata fursa ya kubadilisha mawazo na wale waliowakuta hapo:
Ikiwa ndiyo dakika za lala salama kuelekea kilele cha upigaji kura, wagombea wanaendelea kuongeza kasi za kampeni zao, na mgombea mwingine wa Chama cha Wananchi, CUF, Prof. Ibrahim Lipumba ,yuko katika eneo la kanda ya kaskazini ambako anakosisitiza sera zake za kuwakomboa kiuchumi wananchi.
Mbali ya wagombea hao wa urais kuendelea kuwashawishi wapiga kura, nao wagombea wenza wameendelea kujishughulisha kwa karibu na kampeni hizi wakionekana kuzunguka katika maeneo mbalimbali.
Kuhusu maandalizi ya uchaguzi wenyewe, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC, hivi karibuni iliashiria kukamilika kwa kiwango kikubwa na kinachosubiriwa sasa ni hiyo tarehe 28 ambako wale wenye sifa ya kupiga kura watakapofanya maamuzi yao kwenye sanduku la kura kuchaguwa rais, wabunge na madiwani kwa upande wa Tanzania Bara, huku Zanzibar wakichaguwa pia rais wa visiwa hivyo na wajumbe wa baraza la wawakilishi.