Kampeni za uchaguzi Kenya zashika kas
15 Julai 2022Wakati huohuo, Azimio la Umoja One Kenya Alliance inahitimisha kampeni za siku tano katika eneo la pwani. Kenya Kwanza imepiga kambi eneo la Kiambu kunadi sera zao. Yote hayo yakiendelea, rais Uhuru Kenyatta ameanza rasmi kampeni kumpigia debe Raila Odinga.
Hii leo kambi ya Kenya Kwanza imejikita kaunti ya Kiambu kuwashawishi wapiga kura kuwapa nafasi ya kuwaongoza ifikapo Agosti.Ijapokuwa hali ya hewa hairidhishi, wafuasi walipambana na baridi kali na kufika mjini Lari kuwasilikiza.William Ruto anaipeperusha bendera ya urais.
Kauli hizo zinatolewa saa chache baada ya kiongozi wa taifa kulivalia njuga suala la kumpigia debe mgombea wa urais wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga.Tayari ikulu ya Nairobi imethibitsha kuwa ratba inaandaliwa ya maeneo atakakozuru kumnadi mwanasiasa huyo mkongwe.
Wakati huo huo Azimio la Umoja One Kenya linahitimisha kampeni za siku tano kwenye eneo la pwani.Hii leo wakiwa kaunti ya Kilifi waliahidi kuyabadili maisha ya wakazi wa pwani inayoaminika kuwa ngome yao.
Kwa upande mwengine, tume ya uchaguzi ya IEBC inasisitiza kuwa matokeo yatakayotangazwa ni yale ambayo yamechapishwa kwenye fomu maalum za kuhesabia kura.Tofauti na ilivyokuwa kwenye uchaguzi mkuu uiopita, matokeo yatakayowasilishwa kwa kituo kikuu cha kuhesabia kura kupitia ujumbe mfupi sio yatakayotumiwa kuwatangaza washindi. Kadhalika, IEBC inafafanua kuwa endapo changamoto za kiufundi zitatokea maafisa wake watalazimika kusogea hadi kwenye maeneo yaliyo na mtandao ili kuhitimisha majukumu yao.
Yote hayo yakiendelea, mahakama kuu imefutilia mbali uamuzi wa kupiga marufuku matumizi ya misemo ya hatupangwingwi na watajua hawajui wakati wa kampeni za uchaguzi.Tume ya maridhiano na uwiano wa kitaifa ilishauri misemo hiyo kutotumika kwa msingi kuwa ni kauli za uchochezi.Kulingana na mahakama hakuna ushahidi wa hilo.Zimesalia siku 24 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.
Thelma Mwadzaya DW Nairobi.