Kampeni za uchaguzi Kongo zinakamilika rasmi leo
18 Desemba 2023Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa wito kwa mamlaka za Kongo kuchunguza haraka na bila upendeleo matukio ya vurugu yanayohusiana na uchaguzi na kuwashtaki waliohusika, bila ya kujali waliohusika wanaegemea upande gani wa kisiasa.
Mtafiti mkuu wa Human Rights Watch tawi la Kongo Thomas Fessy ameeleza kuwa, shirika hilo limeorodesha matukio kadhaa ya vurugu kote nchini humo kati ya wafuasi wa vyama hasimu vya kisiasa ambayo yamesababisha mashambulizi ya kulipa kisasi, unyanyasaji wa kingono na kifo cha mtu mmoja.
Inaelezwa kuwa zaidi ya watu milioni 1.5 hawataweza kushiriki zoezi la kupiga kura katika maeneo yenye mizozo, hasa katika jimbo la Kivu Kaskazini na jimbo la magharibi la Mai-Ndombe.
Pia mamilioni ya wakimbizi wa ndani pia huenda wasishiriki zoezi hilo.
Upinzani umeonyesha wasiwasi wao juu ya udanganyifu katika kura huku wakiishtumu serikali kwa kula njama na tume ya uchaguzi CENI na mahakama ya katiba, ambayo ndio msuluhishi wa mwisho wa migogoro ya uchaguzi.