Kampeni za uchaguzi Tanzania zaelekea ukingoni
19 Oktoba 2020Tayari kimefashanya kampeni katika majimbo zaidi ya 10 kati ya 35 yaliyopo kanda hiyo huku duru zikieleza kuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo pamoja na kiongozi wa taasisi ya kiisalmu Shehe Ponda Issa Ponda wataungana na Tundu Lissu katika baadhi ya majukwaa.
Tundu Lissu ambaye kwa sasa anafanya kampeni zake kwa kutumia usafiri wa anga yaani helkopta, anaonekana kupata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wafuasi wanaokwenda kumsikiliza katika maeneo mbalimbali ambayo ameshapita kufanya kampeni katika eneo hili la mikoa ya kanda ya kaskazini, linalotajwa kuwa na siasa ngumu na zenye ushindani mkubwa.
Akiwa katika jimbo la Karatu mkoani Manyara, mgombea huyo aliwahakikishia wafuasi wake kuwa Chadema ipo pamoja na watanzania.
Lissu anaongozana na katibu mkuu wa shura ya maimamu Tanzania Shehe Ponda Issa Ponda ambaye mara kadhaa katika majukwaa ya siasa amekuwa akisisitiza kuwa anamuunga mkono mgombea huyo wa Chadema na chama chake, kwa kuwa ameona chama hicho kinapigania haki na maslahi ya watanzania.
Uwepo wa shehe Ponda katika majukwaa ya siasa kwenye kampeni za Chadema katika dakika hizi za lala salama, unatajwa kuubadilisha kabisa upepo wa siasa nchini.
Leo mgombea wa CHADEMA anamaliza kampeni zake katika jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, na ataendelea tena na ratiba za kampeni kesho katika baadhi ya majimbo ya mkoa wa Arusha.
Mpaka tunakwenda mitamboni mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad bado hajapanda jukwaani kama ratiba ilivyotolewa awali.
Huku hayo yakiendelea mgombea uraisi kupitia chama tawala CCM Dr. John Pombe Magufuli anatarajiwa kufanya mkutano wa kampeni jijini Arusha siku ya tarehe 23 mwezi huu wa Oktoba.
Mwandishi: Veronica Natalis DW Arusha.