1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za Uchaguzi wa urais zamalizika nchini Ufaransa

22 Aprili 2017

Kampeni za uchaguzi wa Rais nchini Ufaransa zimemalizika huku ukiwepo wasiwasi juu ya hali ya usalama baada ya kufanyika mashambulio ya kigaidi mjini Paris.

https://p.dw.com/p/2biT9
Kombobild Macron Le Pen

Hatua za mwisho za kampeni hizo ziligubikwa na mauaji ya polisi kwenye eneo maarufu la Champs Elysees katikati ya mji wa Paris. Wagombea wakuu wanne wataingia katika duru ya kwanza inayotarajiwa kuwa kali hapo kesho hata hivyo kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wapiga kura wengi bado hawajaamua juu ya nani wa kumpa kura zao.  Utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la Elabe kwa niaba ya kituo cha televisheni cha BFM, mgombea anayewakilisha siasa za mrengo wa kati Emmanuel Macron anatarajiwa kushinda kwa kupata asilimia 24 ya kura, wakati mjumbe wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen anatazamiwa kufikia asilimia 21.5 ya kura.

Mjumbe wa chama cha kihafidhina Francois Fillon anafuatia katika nafasi ya tatu kwa kukadiriwa kupata asilimia 20 ya kura. Kiongozi wa mfungamano wa mrengo wa shoto Jean- Luc Melenchon anatarajiwa kushika mkia kwa kupata asilimia 19.5.  Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni Macron mwenye umri wa miaka 39 anatabiriwa kushinda katika duru ya pili kwa kupata asilimia 65, wakati mshindani wake mkuu Marine Le Pen anatazamiwa kupata asilimia 35 ya kura.  Hata hivyo kwa mujibu wa uchunguzi mwingine wa maoni ikiwa kiongozi wa mfungamano wa mrengo wa shoto Melenchon atafanikiwa kuingia katika raundi ya pili ataweza kuwashinda Le Pen na Fillon kwa urahisi lakini atapitwa na Macron.

Frankreich Wahlkampf Emmanuel Macron
Mgombea urais nchini Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Getty Images/S. Lefevre

Uchunguzi uliofanywa na shirika la Elabe unaonyesha kwamba asilimia 25 ya wapiga kura nchini Ufaransa bado hawajaamua juu ya jinsi watakavyo piga kura, wakati huo huo utafiti mwingine umeonyesha wapiga kura ambao bado hawajakata shauri wanafikia asilimia 40. Hata hivyo inapasa kutilia maanani kwamba uchunguzi huo wa shirika la Elabe ulifanyika kabla ya kutokea mashambulio ya kigaidi ya mjini Paris ambapo polisi mmoja aliuwawa na wengine wawili walijeruhiwa. 

Mgombea wa chama cha mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen ameyaambatanisha mashambulio hayo na swala la uhamiaji.  Le pen ameshauri kuwavua uraia wote wenye nasaba za uhamiaji wanao tuhumiwa kuhatarisha usalama wa Ufaransa.  Le Pen aliwaambia waandishi wa habari kwamba ugaidi ni vita vinavyo walenga wananchi na nchi yao yote ya Ufaransa.  Amesema Ufaransa haina budi kushinda vita hivyo.  Mwanasiasa huyo ametamka kwamba itikadi kali ya Kiislamu na itikadi ya Kisalafi hazina haki ya kuwapo nchini Ufaransa na zinapaswa kupigwa marufuku. Mwanasiasa huyo wa mrengo mkali wa kulia ametaka wale wanao hubiri chuki wafukuzwe nchini Ufaransa na misikiti yao ifungwe.

Naye mgombea mwenye siasa za mrengo wa kati Emmanuel Macron ameshauri kuwapo utulivu badala ya kuwachanganya watu kwa kuitumia kadhia  ya ugaidi. Macron aliwaambia waandishi wa habari kwamba lengo la magaidi ni kuiyumbisha Ufaransa wakati ambapo wananchi wake wanauchagua mustakabali wao.

Waziri mkuu wa Ufaransa Bernard Kazeneuve alitangaza hapo jana kwamba polisi zaidi ya alfu 50 na wanajeshi alfu 7 watawekwa kulinda usalama hapo kesho wakati wananchi watakapo shiriki katika kupiga kura kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais.  Wagombea 11 kutoka mirengo yote ya kisiasa wanawania nafasi ya urais katika uchaguzi unaozingatiwa kuwa kipimo cha mvuto wa siasa za kujijengea umaarufu kwa kutumia hoja za kijuu juu na za kuwachota watu mawazo.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/DW

Mhariri:  Sudi Mnette