Kampeni za uchaguzi zakumbwa na vurugu Burundi
6 Mei 2020Mwanasheria Mkuu Sylvestre Nyandwa ameonya wasiasa watachukuliwa hatua kali za kisheria iwapo watasababisha usalama kuharibika.
Akiwahamasisha wafuasi wa chama chake Kathy Nkezimana mgombea ubunge kwa tikiti ya chama cha upinzani CNL aliyekamatwa na kufungwa jela muda mfupi baada ya kuendesha kampeni katika tarafa ya Mugongomanga mkoani Bujumbura vijijini, alisema kamwe hawatowasahau watu waliouwawa na kuitoroka nchi.
"Hatuwezi kuwasahau watu wetu wengi waliouwawa na wengine kuikimbia nchi, ambao wanaendelea kuhangaika makambini Tanzania. Msirudi kuwa na hofu atakayewaanza basi mjihami," alisema Kathy Nkezimana mgombea ubunge kwa tikiti ya chama cha upinzani CNL.
Kufuangwa mgombea huyo kumefuatia makabiliano ya kutumia mapanga kati ya wafuasi wa chama CNL na vijana Imbonerakure wa chama CNDD-FDD, ambapo mfuasi mmoja wa chama cha CNL aliuwawa na wengine wa 8 kujeruhiwa katika tarafa ya Ntega mkoani Kirundo kaskazini mwa nchi.
Rwasa atoa amri ya wafuasi wake kujihami ili kujikinga na mashambulizi
Agathon Rwasa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho CNL aliamrisha wafuasi wake kujihami endepo watashambuliwa. Na kwamba tayari visa vya makabiliano kati ya wafuasi wa vyama hivyo viwili vimeshuhudiwa katika mikoa ya Ngozi, Kayanzam Gitega na Bujumbura vijijini.
Pierre Nkurukiye msemaji wa polisi wa Burundi ameikosoa kauli ya mkuu wa chama CNL kwa kusema Polisi ya taifa imekituhumu chama cha upinzani CNL kwa kutowa matamshi ya kufufua na kuchochea chuki.
"Mkuu wa chama CNL ametowa kauli hiyo mara mbili ya kuwataka watu kukabiliana, na kuchukiana. Na tayari wafuasi wake wamekuwa wakitowa pia kauli hiyo. Hiyo ni kauli waliyokuwa nayo wafuasi wa chama hicho tangu miaka hiyo. Na tayari watu wamepigana, wapo waliokufa na wengine kujeruhiwa. Baadhi ya wahusika tayari wamekamatwa," alisema mkuu huyo wa polisi wa Burundi Pierre Nkurukiye.
Mwanasheria mkuu wa Jamuhuri Sylvestre Nyandwa ametowa onyo kali na kuwakumbusha wanasiasa kuwa sheria inaendelea kufanya kazi hata wakati huu wa kampeni. Na kwamba watakaohusika na kuyumbisha usalama basi sheria itafuata mkondo wake.
Onyo hilo limetolewa pia ma waziri wa mambo ya ndani wa Burundi Pascal Barandagiye. Wakati kampeni za uchaguzi wa Mei 20 zikiendelea malumbano yanadhihirika kuwa makali kati ya chama tawala cha CNDD-FDD na CNL chama maarufu cha upinzani nchini humo.
Chanzo: Amida ISSA, DW Bujumbura