1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi zapamba moto

13 Agosti 2013

Kampeni za uchaguzi mkuu na jinsi zinavyogubikwa na kashfa ya upelelezi, na hali nchini Misri ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

https://p.dw.com/p/19OXu
Kauli mbiu ya kampeni ya uchaguzi ya chama cha CDUPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie na kashfa ya upelelezi na jinsi inavyogubika kampeni za uchaguzi mkuu ujao.Gazeti la "Die Tagepost linakosoa jinsi vyama vya kisiasa vinavyoishughulikia kashfa ya upelelezi humu nchini.Gazeti linaandika:

Haikubaliki hata kidogo jinsi serikali kuu na upande wa upinzani wanavyojishughulisha na kashfa ya upelelezi ya shirika la Upelelezi la Marekani NSA:Badala ya serikali na bunge kuwaeleza wananchi kikamilifu kuhusu harakati za shirika la NSA nchini Ujerumani,shirika la upelelezi la Ujerumani BND limechangia kwa kiasi gani,ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili ni wa aina gani na mipaka ya uhusiano huo inakutikana wapi,serikali na upande wa upinzani wanaitumia kadhia hiyo,kwa kila mmoja kumchafulia sifa mwenzake katika wakati huu wa kampeni za uchaguzi.Hali hiyo sio tu inasababisha ukosefu wa hali ya uwazi linapohusika suala la kuhifadhiwa data ,hali hiyo inadhuru pia imani ya wananchi kwa vyama vya kisiasa.

Kashfa ya Upelelezi inagubika pia kampeni za uchaguzi

Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" linamulika kampeni za uchaguzi mkuu na jinsi juhudi za upande wa upinzani wa SPD zinavyoshindwa kufua dafu.Gazeti linaandika:

Zimesalia wiki chini ya sita kabla ya uchaguzi mkuu.Mpaka sasa lakini hujuma zote hazikusaidia kitu.Suala linalozuka ni kwanini?Kwasababu Merkel ameilaza nchi nzima na SPD hawawezi kuwazinduwa wapiga kura.Merkel binafsi anakwepa malumbano na vyama ndugu vya CDU/CSU vinafanya vivyo hivyo.Na kwanini Merkel ajiingize katika mjadala kuhusu matatizo ambayo kwa maoni ya wananchi walio wengi hayapo?Ikiwa nafasi za kazi zinadhaminiwa,mgogoro wa madeni umeshamalizika na umaskini hakuna au ni fichu?Hapo bila ya shaka anaetaka ataendelea kulala.

Gazeti la "Rhein-Neckar-Zeitung" lina maoni sawa na hayo na kuandika:

Nawafanye watakavyo wana SPD,lakini kansela anaekwepa malumbano anaweza mwishowe kuwa mshirika mwema.Hivyo ndivyo baadhi ya viongozi wa SPD wanavyoiangalia hali ya mambo.Lakini wapiga kura gani wanaohisi hivyo?

Patashika ya Misri

Hali nchini Misri nayo pia imemulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.Gazeti la "Münchner Kurier" linaandika:

Ni sawa kabisa kwamba Mursi ni mfuasi wa Udugu wa kiislam na kiongozi ambae wafuasi wengi wa itikadi kali wanamuwekea matumaini lakini yeye pia ni rais wa kwanza wa nchi hiyo aliyechaguliwa kwa njia huru.Wanajeshi wakimwachia huru,basi wafuasi wa itikadi kali wataiangalia hali hiyo kuwa ni ushindi kwao.Kama hawatomtoa,basi maandamano yanaendelea na nchi za magharibi hazitakosea zitakaposhuku kama kweli wenye kudhibiti madaraka katika nchi hiyo ya mto Nile wana hamu ya kuleta mageuzi ya kidemokrasia.Ishara ya ufumbuzi haijachomoza.Na kiongozi mwenye ushawishi wa kutosha na haiba kuweza kutuliza hali ya mambo,nae pia haonekani.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef