Kenya: Kampeni zamalizika malumbano yaendelea mitandaoni.
7 Agosti 2022Wafuasi wa wagombea wakuu kwenye uchaguzi ujao wanatumia mitandao kuendeleza tuhuma juu ya wagomea wa upande mwingine kushiriki kwenye visa vya udanganyifu.
Benedict Manzin, mchambuzi wa maswala ya kisiasa ya eneo la Afrika, kusini ya Jangwa la Sahara katika kampuni ya kijasusi ya Sibylline yenye makao yake Uingereza amesema wafuasi wa Naibu Rais, William Ruto na wale wa mwanasiasa mkongwe Raila Odinga, wanasambaza taarifa nyingi zinazodai kuwa wapinzani wao wanajihusisha na "njama za wizi wa kura".
Mashirika ya kiraia nchini Kenya na shirika la uangalizi yameonya kwamba taarifa hizo potofu zinahatarisha demokrasia na yameyataka majukwaa ya mitandao ya kijamii kuchukua hatua. Serikali ya Kenya pia imeanzisha kitengo maalum cha kushughulikia makosa ya uchaguzi na matamshi ya chuki.
Mashirika makuu ya habari pia yametumbukizwa kwenye sintofahamu hiyo, wakati ambapo tovuti za walaghai na kurasa zao za mitandao ya kijamii zikichapisha taarifa ghushi zinazoeneza uwongo kuhusu wagombeaji na kuzifanya zionekane kama ni matangazo halisi.
Soma Zaidi:Uchaguzi Kenya 2022: Kampeni za uchaguzi zamalizika leo
Mhariri wa Citizen TV Waihiga Mwaura amesema wanalazimika kutoa arifa kila mara na kubainisha kuwa taarifa hizo hazikutoka kwenye kampuni yao.
Kura za maoni za ulaghai zimeibuka kuwa ni mtindo mkuu, huku wazushi wa taarifa za uwongo wakizihusisha na vyanzo halali kama vile kampuni ya uchunguzi ya GeoPoll na gazeti la The Daily Nation.
Allan Cheboi, mpelelezi mkuu wa Code for Africa mpango unaoshughulikia teknoljia ya habari wa data za raia amesema wahusika wa majukwaa kama Facebook na TikTok ingawa wanasema wamejipanga kuziondoa taarifa potofu na matamshi ya chuki lakini kuna shaka kwa sababu washawishi wa uchaguzi wanatumia maneno ya siri ili kufikisha ujumbe wao. Amesema zipo lugha nyingi za kificho zinazotumika ambazo mitandao hii ya kijamii haiwezi kuzitambua kama ni matamshi ya chuki. Ameongeza kusema kuwa uchochezi huanza mtandaoni na kisha husababisha vurugu halisi nje ya mtandao.
Angalia:
Mary Blankenship, mtafiti wa habari za kupotosha katika Chuo Kikuu cha Nevada, amesema madai yasiyo na msingi ya wizi wa kura, yanaweza kusababisha madhara makubwa, hasa katika nchi ambayo uchaguzi uliopita ulikumbwa na ghasia.
Wakenya watapiga kura ya kumchagua Rais, wabunge na viongozi wengine siku ya Jumanne tarehe 9 Agosti. Mshindi katika uchaguzi huo atamrithi Rais Uhuru Kenyatta anayemaliza muda wake baada ya kuiongoza Kenya kwa mihula miwili. Wachambuzi wanasema ushindani ni mkali mno kati ya wagomea wawili wakuu na kwamba kwa mara ya kwanza nchini Kenya inawezekana kufanyika duru ya pili ya uchaguzi nchini humo.
Chanzo:AFP