1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni zaendelea kupamba moto Tanzania

Hawa Bihoga 28 Septemba 2020

Kampeni za uchaguzi mkuu zimeendelea nchini Tanzania ambapo chama tawala CCM kimeanza awamu ya tatu ya kampeni zake baada ya mgombea wake John Magufuli kupumzika kwa siku kadhaa.

https://p.dw.com/p/3j7gH
Tansania Dar es Salaam | Wahlplakate
Picha: Eric Boniphace/DW

Chama cha upinzani cha TADEA nacho kimezindua kampeni zake na kutoa kipaumbele katika utawala bora endapo kitachukua uongozi wa dola hapo Oktoba 28.

Ni takriban siku 30 zikiwa zimesalia zoezi la kampeni kufungwa rasmi kwa mujibu wa ratiba ya tume ya taifa ya uchaguzi, chama tawala CCM, kimeanza kampeni zake katika awamu ya tatu huku kikiweka hadharani kutumia hazina yake ya viongozi waandamizi wa chama na taifa katika kumnadi mgombea wa chama hicho dokta John Magufuli.

Katika ukanda wa nyanda za juu kusini katika mkoa wa Iringa, CCM inamtumia waziri mkuu mstaafu wa awamu ya nne na mjumbe wa halmashauri kuu Mizengo Pinda katika kuwahamasisha wapiga kura mkoani humo kumpigia kura Rais John Mgufuli na na wabunge wote wa chama chake.

Soma pia: Tume ya uchaguzi Tanzania yamuita Lissu kujieleza

Polisi Tanzania yasema msafara wa Lissu haukushambuliwa

Akiwahutubia wapiga kura amesema, tayari ameanza kutekeleza miradi kadhaa ya kitaifa kwa ajili ya maendeleo iliolenga katika sekta ya afya, elimu, miundombinu ikiwemo nishati.

Hivyo kuwaomba wanairinga kumpigia kura ili aendeleze  maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla na hatimae kufikia lengo la uchumi wa nchi kukua kwa asilimia 8 kutoka asilimia 7 kwa kipindi hiki. 

Chama cha wananchi CUF ambacho nacho kikionekana kuwa miongoni mwa vyama ambavyo vinachuana vikali na chama tawala CCM kupitia mgombea wake ambae ni mtaalamu wa uchumii Profesa Ibrahim Lipumba anaendelea na kampeni zake katika mikoa ya kanda ya ziwa ambako amezungumza na wapiga kura katika mkoa wa Geita akiwasisitiza kuwa kuna haja ya rasilimali za madini kuendelea kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa na mikataba bora ya madini kwa maslahi ya umma.

Kampeni na siasa nchini Tanzania zapamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.
Kampeni na siasa nchini Tanzania zapamba moto kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.Picha: DW/S. Khamis

Hoja ya utawala bora nayo inaendelea kutikisa kampeni hizi za uchaguzi ambapo chama cha ADA TADEA inaibeba hoja hiyo miongoni mwa hoja zake za kuelekea ikulu kwa kutumia utawala wa sheria na kuheshimu kila muhimili katika nchini, huku kikudumisha amani na utulivu kwa maendeleo ya umma.

Siku ya Jumanne, Rais Magufuli anatarajiwa kuendelea na kampeni zake huko mkoani Iringa eneo ambalo siasa zake zinatazamwa kuwa na mvutano mkali kutokana na jimbo la Iringa mjini kuongozwa na upinzani kwa kipindi cha miaka 10.