Kansela Merkel atoa mwito wa uchaguzi huru Syria
28 Oktoba 2018Mkutano huo wa kilele uliwaleta pamoja Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Rais wa Urusi Vladimir Putin, na mwenyeji wao, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki. Kwa pamoja viongozi hao waliazimia kutafuta mwafaka kuhusu namna hali ya amani inavyoweza kurejea Syria.
Baada ya mazungumzo yao, Kansela Merkel alihimiza kuwepo kwa mchakato wa kisiasa wa kumaliza uhasama nchini Syria, ambao utasimamiwa na Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kufikia uchaguzi huru.
''Baada ya mchakato huo, kunapaswa kufanyika uchaguzi huru utakaowahusisha raia wote wa Syria, wakiwemo walioko nje ya nchi,'' alisema Merkel katika mkutano na waandishi wa habari.
Katiba mpya kwa Syria
Wito huo wa Kansela Merkel uliungwa mkono katika tangazo la pamoja lililotolewa na Rais Erdogan na viongozi wengine. Katika tangazo hilo, Erdogan alisema, ''Tumetoa mwito wa kuwepo haraka iwezekanavyo, mchakato wa kuunda kamati ya katiba, ikiwezekana kabla ya kumalizika mwaka huu.''
Aidha, tangazo hilo la pamoja limegusia tatizo la wakimbizi na kuheshimisha usitishwaji wa mapigano katika mkoa wa Idlib. Mkoa huo ulio Kaskazini Magharibi mwa Syria, ndio eneo pekee muhimu linalosalia chini ya udhibiti wa waasi.
Mwezi uliopita, Urusi na Uturuki zilikubaliana kuhusu ukanda usio na shughuli za kijeshi kuuzunguka mkoa huo, lakini ghasia zilishamiri kabla ya mkutano wa jana. Rais Putin hata hivyo amesema kwamba Uturuki inaheshimu upande wake wa makubaliano.
Rais Emmanuel Macron alisisitiza umuhimu wa kusitisha mapigano: ''Tutakuwa macho kabisa kuhakikisha kwamba kila upande unatekeleza wajibu wake, ili makubaliano ya kusitisha mapigano yaendelee kuwa imara,'' alisema kiongozi huyo.
Assad sio 'mwaminifu'
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alitumia fursa ya mkutano huo kumkosoa Rais wa Syria Bashar al-Assad, akisema sio mtu wa kuaminika.
''Raia wa Syria waliokon ndani na wa nje, ndio watakaoamua hatma ya Assad, sio mtu mwingine,'' alisema Erdogan na kuongeza kwamba hawezi kumuamini Assad aliyemtuhumu kuuwa watu milioni 1.
Vita vya Syria vilivyoanza mwaka 2011 na bado vinaendelea. Watu zaidi 360,000 wamepoteza maisha katika vita hivyo, na mamilioni wengine wameingia ukimbizini.
Kivuli cha Khashoggi
Mkutano wa kilele wa Jumamosi mjini Istanbul ulifanyika huku Rais Macron na Kansela Merkel wakiendelea kutofautiana vikali kuhusu mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia, baada ya kuuawa kwa mwandishi wa habari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia. Wakati Merkel aliamua kusitisha mauzo hayo, Macron amesema hatua ya Merkel ni ya kufuata mkumbo.
Licha ya tofauti hizo lakini, ofisi ya Macron imesema viongozi hao wawili wamekuwa na mazungumzo mazuri katika mkutano wa Istanbul, na wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika ngazi ya Ulaya kuhusu suala la Saudi Arabia.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, dpae
Mhariri: Yusra Buwayhid