1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel kukutana na rais Sarkozy mjini Paris leo

5 Desemba 2011

Leo mchana, Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy anamkaribisha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Paris ambako viongozi hao wawili, wanatazamiwa kuafikiana kuhusu mpango wa kuiokoa sarafu ya euro.

https://p.dw.com/p/13N8O
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais Nicolas Sarkozy wa UfaransaPicha: dapd

Ujerumani na Ufaransa zinazobeba jukumu kuu la kutafuta suluhisho kwa mzozo huo wa euro barani Ulaya, leo mchana, zinatazamiwa kuyakamilisha mapendekezo ya mpango utakaowasilishwa kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya baadae wiki hii mjini Brussels. Lengo la mkutano wa leo ni kuondosha tofauti zilizopo kabla ya kufanyika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya mwishoni mwa wiki hii mjini Brussels.

Hata hivyo, Merkel na Sarkozy waliopewa jina "Merkozy" wanakubaliana kuhusu mageuzi ya kufanywa katika mkataba wa Umoja wa Ulaya ili kuweza kuwa na ukaguzi mkali wa nidhamu katika matumizi ya serikali za kanda ya euro. Nchi zinazokwenda kinyume na masharti yaliyokubaliwa zichukuliwe hatua kali.

Wakati huo huo, Merkel anapendekeza kuimarisha mamlaka ya taasisi za Ulaya ili ziweze kuingilia kati bajeti za taifa. Lakini Sarkozy anapinga kabisa kuzipa taasisi hizo mamlaka makubwa kama hayo. Yeye anaunga mkono dhamana za pamoja za kanda ya euro - maarufu kama "Eurobonds" lakini Merkel anasema, hiyo kwa sasa wala haitosaidia kuudhibiti mzozo wa sarafu ya euro. Ujerumani iliyochoka kutoa misaada mikubwa ya fedha mara kwa mara kuziokoa serikali zenye madeni katika kanda ya euro, sasa inataka mageuzi ya kimsingi katika mkataba wa Umoja wa Ulaya.

Lakini hata kama mageuzi yanayopendekezwa yataidhinishwa kwenye mkutano wa viongozi mjini Brussels, itachukua zaidi ya mwaka mmoja kuibadili katiba. Hata hivyo, wataalamu wengi wa masuala ya kiuchumi, wana hofu kuwa kanuni mpya pekee hazitosaidia kuzuia gharama za mikopo zinazozidi kuongezeka katika nchi za Ulaya.

Lakini hata ishara ya kuwepo nia ya kufanya mageuzi hayo itaitia moyo Benki Kuu ya Ulaya ECB na hivyo itajitahidi zaidi kutoa msaada kwa muda mfupi. Hivyo, serikali zenye madeni, zitapata wakati wa kuzidhibiti bajeti zake na kufanya mageuzi ya kiuchumi yatakayosaidia ukuaji.

Hii ni wiki muhimu sana kwa sarafu ya euro. Leo thamani ya  euro imepanda katika masoko ya fedha yalio na matumaini kuwa viongozi wa Ulaya  baadae wiki hii mjini Brussels wataukubali mpango wa kuumaliza mzozo wa madeni unaoendelea tangu miaka miwili barani Ulaya.

Mwandishi:Martin,Prema/rtre/dpa

Mhariri:Josephat Charo