Kansela Merkel tosha kwa uchaguzi 2017
3 Aprili 2017Kura ya maoni iliyofanywa na kampuni ya Forsa imeonyesha kuwa licha ya umaarufu wa Merkel kupungua kutokana na sera yake ya milango wazi kwa wakimbizi asilimia 59 ya Wajerumani bado ina imani nae. Japo wandani wa kansela Merkel wamesema wanatazamia kuwa atagombea tena nafasi hiyo mwaka ujao wa 2017 chini ya muungano wa kihafidhina, yeye mwenyewe amekataa kuzungumzia hilo , akisema atatoa tamko wakati muafaka. Hata hivyo asilimia 35 ya Wajerumani imechoshwa na utawala wa mwanasiasa huyo wa muungano wa kihafidhina kwa mujibu wa kura hiyo ya maoni. Muuungano huo wa kihafidhina unavileta pamoja chama cha Christian Democratic Union -CDU chake Merkel, na chama cha Christian Social Union-CDU kinachotawala jimboni Bavaria.
Merkel mwenye umri wa miaka 62 ameiongoza Ujerumani tangu mwaka 2005.Siasa za uchaguzi huo mkuu hata zimesababisha mpasuko katika chama cha watetezi wa mazingira die Grüne, kufuatia mgogoro wa iwapo chama hicho kijiunge katika ushirikiano wa kihafidhina unaoogozwa na Merkel. Ndani ya chama hicho cha kijani wako wanaohisi hatua hiyo itakuwa ni kuzisaliti fikra au muongozo wa chama chao huku wengine wakiiona kuwa jambo zuri.Mgogoro huo uliibuka baada ya kiongozi mkongwe wa chama hicho cha kijani Winfred Kretschmann mwenye umri wa miaka 68 kutoa kauli mwezi huu kuwa Merkel anapaswa kugombea muhula wa nne. Mkongwe huyo wa chama cha kijani ambaye ni waziri mkuu wa jimbo la Baden Wuttenberg alisema hajamuona mtu mwingine yoyote anayeweza kuwa bora zaidi ya Kansela Markel.Kauli hiyo ya kumsifu Angela Merkel ndiyo mzizi hasa ulioibua mgawanyiko pamoja na hali ya fedheha katika ngazi za uongozi wa chama hicho,mvutano ambao unatarajiwa kuchukua tena nafasi kubwa katika mkutano mkuu wa chama hicho hapo kesho ijumaa.Kuna makundi mawili ndani ya chama hicho yanayopishana maneno kuhusu pendekezo hilo.Kundi la kwanza likiwa la wale wanaotazama mambo katika uhalisia wake na upande wa pili likiweko lile la msimamo mkali. Makundi hayo yatabidi kutafuta msimamo mmoja katika mkutano huo unaoanza kesho juu ya suala hilo. Wanasiasa wa vyama vyote cha kijani na kile cha Kansela Angela Merkel wamekuwa wakizungumzia juu ya kutokea kisichofikiriwa ,ambacho ni ushirikiano katika kuiongoza Ujerumani kati ya chama cha CDU cha Merkel na chama kinachoegemea siasa za mrengo wa kushoto cha wanamazingira.Katika mvutano unaondelea ndani ya chama cha kijani juu ya suala hilo mmoja wa kiongozi mwenza wa chama Simone Peter alisema wanataka kuufikisha mwisho uongozi wa muungano mkuu wa Kasela Merkel na kwahivyo hawawezi kuwa watu sahihi wa kuamua nani anayepaswa kuwa Kansela Mpya.Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Ujerumani kama Lothar Probst kutoka chuo kikuu cha mjini Bremen amesema kujiunga na chama cha Christian Democratic Union bado ni suala linaloibua mkanganyiko ndani ya chama cha kijani lakini sio fikra tena ya kuogofya kwa chama hicho.
Mwandishi: Jane Nyingi/RTRE/AFPE
Mhariri: Iddi Ssessanga