1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani ataka mamluki waondoke Libya

2 Oktoba 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa wito wa kuondolewa mamluki wote nchini Libya kwenye mkutano na rais wa kipindi cha mpito nchini Libya Mohammad Younes Mnefi anayefanya ziara nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/41AJy
Deutschland | PK Angela Merkel und Mohammad Younes Mnefi
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela Angela Merkel amesema mustakabal wa Libya unapaswa kujengwa na watu wa Libya bila ya ushawishi kutoka nje. Merkel pia amesisitita umuhimu wa uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Desemba 24 na ameahidi kuwa Libya itaendelea kupewa kipaumbele katika sera ya nje ya Ujerumani.

Kwenye mkutano wake na rais wa mpito wa Libya Mohammed Minfi, kiongozi wa Ujerumani pia ameahidi kuiunga mkono Libya kiuchumi. Ujerumani ni miongoni mwa nchi zinazosuluhisha katika mgogoro wa nchi hiyo ya Afrika kaskazini. Amesema bado kuna mengi yanayohitaji kufanywa nchini Libya.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Michael Kappeler/AFP

Baada ya kupinduliwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011, Libya iliingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilijumuisha idadi kubwa ya wanamgambo. Makubaliano ya kusimamisha mapigano yalifikiwa tangu mwaka jana na mapema mwaka huu, serikali ya mpito iliundwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa ambayo imepewa jukumu la kuongoza nchi hadi uchaguzi utakapofanyika.

Mwaka jana, serikali ya Ujerumani ambayo imechukua jukumu la kuwa kama mpatanishi katika mzozo huo iliandaa mkutano mkuu mjini Berlin lengo likiwa ni kumaliza hatua za nchi nyingine kuingilia kati mgogoro wa Libya pamoja na uingizaji wa silaha na mamluki nchini humo. Miongoni mwa nchi zilizohusika katika mgogoro wa Libya ni pamoja na Urusi, Uturuki, Misri na Falme za Kiarabu.

Muammar Gadaffi aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa Libya aliyepindulia na kuuawa mwaka 2011.
Muammar Gadaffi aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa Libya aliyepindulia na kuuawa mwaka 2011.Picha: Getty Images/AFP/C. Simon

Libya kwa miaka mingi imekuwa kitovu cha kuwasafirisha wahamiaji kutoka Afrika na Mashariki ya Kati wanaokimbia vita na umaskini katika nchi zao wakitumaini kuanza maisha bora barani Ulaya. Wafanyabiashara haramu ya kusafirisha watu wametumia machafuko ya nchini Libya kujinufaisha kwa kuwasafrisha wahamiaji kwa kutumia boti za mpira au za mbaokupitia bahari ya Mediterrania.

Maelfu ya wahamiaji wamezama na kupoteza maisha huku wengine wakikamatwa na kurudishwa nchini Libya na kuwekwa mahabusu ambako mara nyingi watu hao huteswa na kulazimishwa kutoa fidia.

Chanzo:// AP