Kansela wa Ujerumani asaka nishati kwenye nchi za Ghuba
24 Septemba 2022Kansela Scholz, ambaye ameandamana na ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara wa sekta ya viwanda, alipokelewa katika uwanja wa ndege wa Jeddah na gavana wa eneo la Makkah Mwanamfalme Khalid bin Faisal Al Saud.
Scholz, amekutana na kiongozi wa Saudi Arabia mwanamfalme Mohammed bin Salman na baadae leo Jumamosi Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na ujumbe wake wataelekea Umoja wa Falme za Kiarabu ambako siku ya Jumapili atakutana na Rais wa UAE Sheikh Mohamed bin Zayed Al-Nahyan na Jumapili hiyo hiyo watakwenda Qatar nchi yenye utajiri wa gesi ambako kansela Scholz atafanya mazungumzo na Emir Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani.
Kansela huyo anatumai atafaulu katika kuanzisha ushirikiano mpya utakaowezesha nchi yake kufikia makubaliano mapya ya nishati na mataifa hayo ya Ghuba yenye utajiri wa mafuta na gesi, ili kuziba pengo la nishati kutoka Urusi tangu nchi hiyo ilipoanza uvamizi wake nchini Ukraine.
Hata hivyo kansela Scholz anakabiliwa na mtihani wa kusawazisha maswala ya kidiplomasia, kwani atalazimika kuepuka tofauti kubwa na wenyeji wake kuhusu haki za binadamu.
Hadi hivi karibuni, Mwanamfalme Mohammed bin Salman alitengwa na Marekani na nchi za Magharibi kutokana na kuuliwa kwa mwandishi wa Habari Jamal Khashogi wa jarida la Washington Post aliyeukosoa utawala wa kifalme mnamo mwaka 2018.
Serikali ya Ujerumani ililaani vikali mauaji ya mwanahabari huyo na hata kabla ya kansela kuanza ziara yake vyanzo katika serikali yake vilisema Ujerumani haitabadili msimamo wake kuhusiana na hilo.
Hata hivyo chanzo kimoja kutoka serikalini kimeeleza kwamba Saudi Arabia kama nchi muhimu inayouza mafuta na yenye nguvu kubwa katika kanda ya mashariki ya kati inamaanisha pana ulazima wa kuwa na uhusiano thabiti na mwana mfalme Mohamed bin Salman.
Chanzo hicho cha serikali kimesema lazima Ujerumani ifanye kazi na Saudi Arabia ikiwa inataka kusuluhisha, kwa mfano, vita vya nchini Yemen au kushughulikia suala la Iran miongoni mwa maswala mengine.
Ujerumani inataka kuupanua ushirikiano katika teknolojia mpya kama hidrojeni ya kijani inayozalishwa kwa kutumia nishati mbadala, ambayo Ujerumani inaweza kuagiza kwa wingi kutoka mataifa ya Ghuba.
Vyanzo vya serikali vinasema kansela Scholz anatakiwa kuimarisha ushirikiano wa kisiasa na mataifa yenye nguvu katika kanda ya Mashariki ya kati, yanayovutwa kwa upande mwingine na Urusi na China.
Vyanzo:AFP/DPA