Karadzic kupelekwa katika mahakama ya The Hague wikendi hii
24 Julai 2008Kuwasilishwa kwa Radovan Karadzic hakutafanyika haraka kama ilivyotarajiwa. Kiongozi huyo anaelezwa kuwa mmoja wa watu waliotafutwa sana ulimwenguni na mhalifu mkubwa wa kivita barani Ulaya tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.
Kesi inayomkabili Radovan Karadzic huenda ikamalizika haraka kuliko kesi nyengine za uhalifu wa kivita mjini The Hague kwa kuwa kiongozi huyo wa zamani aliyejibadili sura anapitisha maamuzi kama aliyopitisha kiongozi wa zamani wa Serbia Slobodan Milosevic. Karadzic amesema anataka kujitetea mwenyewe.
Katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague nchini Uholanzi magari yanayotumiwa kurushia matangazo ya televisheni tayari yamejipanga yakiwa na vifaa vya satelite. Timu za wapigaji picha na waandishi habari kutoka ulimwenguni kote wanasubiri kwa hamu kubwa kuwasili kwa Radovan Karadzic katika mahakama hiyo. Mara tu atakapowasili majaji wanatarajiwa kumsomea mashataka yake mara moja ili kiongozi huyo aungame makosa yake au akanushe mashtaka dhidi yake.
Mara kwa mara huchukua muda wa mwezi mmoja au hata miaka kabla kesi halisi dhidi ya mshtakiwa kuanza katika mahakama ya The Hague. Lakini wakati huu mambo huenda yakaenda haraka kuliko kawaida kama anavyosema Wolfgang Schonburg, jaji pekee mjerumani aliye katika mahakama ya mjini The Hague.
´Tuna ushahidi na habari tulizokusanya ambazo kwa jumla zinaweza kutoa picha nzuri ya kuthibitisha makosa yalifanyika. Jambo la kwanza muhimu ni kuthibitisha jukumu la kibinafsi alilokuwa nalo Radovan Karadzic.´
Kukamatwa kwa Karadzic kwapongezwa
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice leo amepongeza kukamatwa kwa Radovan Karadzic na kusema ana matumaini kamanda wa Karadzic, Ratko Mladic, naye pia atatiwa mbaroni.
Akizungumza na waandishi wa habari wanaoandamana naye katika ziara yake barani Asia, Condoleezza Rice amesema eneo la Balkan limekuwa likijaribu kukabiliana na hali ngumu kwa kipindi kirefu na hivyo kukamatwa kwa Karadzic ni hatua moja kuelekea kumalizika kwa historia mbaya. Aidha waziri Rice amesema kukamatwa kwa Karadzic ni hatua kubwa mbele kwa Serbia na utambulisho wake wa Ulaya.
Hii leo pia Iran imekukaribisha kukamatwa kwa Radovan Karadzic ikikueleza kuwa tukio la kihitoria. Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Iran, Hassan Qashqavi, amenukuliwa na shirika rasmi la habari la Iran, IRNA, akisema kukamatwa kwa Karadzic ni kitendo kisichoweza kusahaulika na kesi ya mauaji ya haliki dhidi ya kiongozi huyo yumkini ikasaidia kupunguza mateso ya jamaa za wahanga.
Iran iliwasaida waislamu wa Bosnia wakati wa vita vya Bosnia kati ya mwaka wa 1992 na 1995. Inakisiwa iliwapa silaha lakini serikali ya Tehran inasema iliwapa tu msaada wa kisiasa na kiuratibu.
Serbia yaanza uchunguzi
Na habari za hivi punde zinasema maafisa wa Serbia wanachunguza ni nani aliyemsaidia Radovan Karadzic kuwa na utambulisho bandia wa Dragan Dabic. Kwa mujibu wa maafisa wa Serbia Dragan Dabic alikufa wakati wa vita vya Bosnia, lakini habari kutoka Sarajevo zinasema alikuwa raia aliyeuwawa na vikosi vya Karadzic vilivyouzingira mji mkuu huo wa Bosnia wakati wa vita vya Bosnia.