1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kasheshe ya ushindi wa Viktor Orban nchini Hungary

Oumilkheir Hamidou
10 Aprili 2018

Vita vya Syria , ushindi wa chama cha kihafidhina cha Hungary cha Viktor Orban na mjadala kuhusu kupigwa marufuku wasichana wenye umri wa chini ya miaka 14 kufunga hijab nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/2vlfQ
Syrien Ost-Ghoua Duma Artilleriebeschuss
Picha: picture-alliance/Xinhua/A. Safarjalani

Tunaanzia Syria ambako hivi karibuni rais wa Marekani Donald Trump alizungumzia uwezekano wa kuwaondowa wanajeshi wa nchi yake akihoji mataifa mengine yanabidi kuwajibika. Hali inazidi kuwa mbaya nchini humo na sasa rais Trump anabadilisha msimamo na kutishia kuichukulia hatua kali serikali ya mjini Damascus. Gazeti la "Die Rheinpfalz" linazungumzia kigeugeu cha rais Trump na kuandika: "Donald Trump yuko madarakani tangu january mwaka 2017. Hajaonyesha dalili yoyote ya kuwa na mkakati wa Syria unaopindukia mapambano dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali wa dini ya kiislam-IS. Rais wa Marekani amezama katika bahari ya ndoto. Anajiambia, vita vitamalizika tu na wao havijawahusu. Hayo si kweli, vita vya Syria vina uhusiano na jukumu la siku za mbele la Marekani ulimwenguni. Kigeugeu cha rais Trump kinabainika anapotaka kwa upande mmoja kuzuwia ushawishi wa Iran katika eneo la mashariki ya kati na upande wa pili akihoji anataka kuwaondowa wanajeshi wake kutoka Syria. Au ni hadaa na badala yake anaitanguliza mbele Israel ili kuwaonyesha Mamullah mipaka yao inamalizikia wapi? Watu wasitegemee mambo kubadilika seuze tangu juzi , mfuasi wa siasa kali za kihafidhina John Bolton ameshakabidhiwa hatamu za uongozi kama mshauri wa masuala ya usalama wa rais Donald Trump."

Ushindi wa Viktor Orban na siasa zake za chuki dhidi ya wageni

Ushindi wa chama cha kihafidhina cha waziri mkuu wa Hungary, Viktor Orban umezusha hisia tofauti miongoni mwa wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Katika wakati ambapo baadhi wanauangalia ushindi huo kuwa ni pigo kwa maadili ya Umoja wa  ulaya, wengine wanahisi  ushindi huo ni uamuzi wa wananchi. Gazeti la "Landeszeitung" linaandika: "Ushindi wa Orban ni kibali alichopewa kuendelea na mkondo wake wa siasa kali za kizaledo na wakati huo huo ni pigo kwa Umoja wa ulaya. Kwamba wanaopigania uzalendo barani Ulaya wanashangiria ushindi wa Orban ni jambo lililokuwa likitarajiwa. Lakini kwamba waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer anashangiria na kufika hadi ya kusema daima amekuwa akiziangalia kuwa ni makosa"sera za kiburi na ubwana  za baadhi ya mataifa mbele ya mataifa mengine, hilo linaumiza. Kiburi mbele ya nani? Mbele ya Orban? Mwanasiasa huyo tangu zamani anatafuta malumbano na Umoja wa ulaya. Anakwenda kinyume na makubaliano kuhusu kinga ya ukimbizi, anauwekea vizuwizi uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa vyombo vya sheria. Kwamba viongozi wa mjini Brussels hawajui wafanye nini, kuna sababu zake. Vyama vya kihafidhina barani Ulaya vinamshangiria kila mbunge wa chama cha Orban anaejiunga na bunge la Ulaya. Mkuu wa kundi la wabunge wa vyama vya kihafidhina katika bunge la ulaya, Weber anafurahi kila anapopata fursa ya kushirikiana na Orban katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoukabili Ulaya. Kwamba Orban mwenyewe ni changamoto, hasemi."

Hijab zipigwe marufuku kwa wasichana wa chini ya miaka 14

Mjadala kuhusu kupigwa marufuku wasichana wenye umri wa miaka 14 kufunga hijabu umehanikiza na hasa katika jimbo hili la North Rhine Westphalia. Mhariri wa gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung" anakumbusha ugumu wa kutekelezwa marufuku hayo na kuandika: "Sio tu hijab, itamaanisha hata suala la watoto  wa kikristo wanaovaa vidani vyenye misalaba lijadiliwe. Katika mjadala huo uliopamba moto watu wanasahau kwamba juhudi za kujumuishwa wahamaji katika maisha ya kila siku ya jamii hazitekelezeki kwa kupiga marufuku hijabu."

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/inlandspresse

Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman