Wapalestina zaidi watoroka eneo la Kaskazini mwa Gaza
8 Novemba 2023Wapalestina hao wametoroka eneo hilo la Gaza huku balozi wa Israel nchini Poland, Yacov Livne akitoa wito kwa watu, taasisi na serikali kusaidia kuachiwa huru kwa mateka 240 wa Israel wanaozuiwa na kundi la wanamgambo Wakipalestina la Hamas.
OCHA yatoa takwimu za Wapalestina waliotoroka Kaskazini mwa Gaza
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, imesema takriban watu elfu 15 walikimbia kutoka eneo hilo hapo jana Jumanne ikilinganishwa na watu elfu 5 walioondoka Jumatatu na wengine elfu 2 waliokimbia eneo hilo siku ya Jumapili mwishoni mwa wiki miliyopita.
Soma pia: Israel yaendelea kuishambulia Gaza angani na ardhini
Eneo la kaskazini la Gaza lenye idadi kubwa ya watu hasa katika mji mkuu, Gaza City na kambi za wakimbizi za mijini zilizo na msongamano mkubwa wa watu, ndizo shabaha za kampeini ya Israeli ya kuliangamiza kundi la wanamgambo la Hamas, ambalo limetawala katika ukanda wa Gaza kwa miaka 16.
Vita hivyo, ambavyo sasa vimeingia mwezi wake wa pili, vilichochewa na shambulizi la kushtukiza la kundi la Hamas Kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7.
Balozi wa Israel kwa Poland atoa wito wa kuachiwa huru kwa mateka wa Israel
Picha za watu waliotekwa nyara leo ziliwekwa mbele ya mnara wa Nicolas Copernicus mjini Warsaw nchini Poland pamoja na nguo, wanasesere au madoli. Mabango katika eneo hilo yaliandikwa ujumbe unaosema ,''usikubali watoto wako wawe wahanga watakaofuata.
Soma pia: Netanyahu: Mapigano hayaishi hadi Hamas iwaachie mateka
Balozi Livne amesema kuwa hakujachukuliwa hatua za kutosha kote ulimwenguni kuwarudisha nyumbani raia wa Israel waliokamatwa mateka na kundi la Hamas.
Livne amesema wanatarajia watu wawe wazi zaidi. wanahitaji wito wa moja kwa moja kutoka kwa shirika la msalaba mwekundu, kutoka kwa kila mmoja anayehusika katika hali hii, kwa kundi la Hamas na wanaohusika wote.
Qatar yasimamia mazungumzo kati ya Israel na kundi la Hamas
Huku hayo yakijiri, Qatar inasimamia mazungumzo kati ya Israel na kundi la Hamas ya uwezekano wa kuachiwa huru kwa mateka kati ya 10 hadi 15 wanaoshikiliwa Gaza ili kubadilishana na kipindi kifupi cha kusitishwa kwa mapigano. Haya ni kulingana na duru iliyoliarifu shirika la habari la AFP hii leo.#
Italia kupeleka meli ya huduma za hospitali Gaza
Katika hatua nyingine, Waziri wa ulinzi wa Italia Guido Crosetto, amesema nchi yake itapeleka meli ya huduma za hospitali karibu na Pwani ya ukanda wa Gaza kusaidia kuwatibu waathiriwa wa mzozo kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas.
Crosseto amesema meli hiyo inaondoka Italia leo ikiwa na wafanyakazi 170 wanaojumuisha watu 30 waliopata mafunzo ya dharura za kimatibabu.
Israel kutoshiriki mazungumzo ya msaada wa kiutu kwa Gaza
Mbali na hayo, ofisi ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, imesema kuwa wawakilishi wa Israel hawatashiriki katika mkutano wa kesho uliopangwa na rais huyo mjini Paris, kuzungumzia msaada wa kiutu kwa Gaza.
Soma pia:Israel kuchukua jukumu la usalama wa Gaza baada ya vita
Afisa mmoja kutoka ofisi hiyo aliyezungumza na waandishi wa habari kwa sharti la kutotajwa, amesema kama serikali nyingine, Israel hata hivyo ina nia ya kuboresha hali ya kibinadamu huko Gaza.
Ikulu ya rais ya Elysee nchini Ufaransa, imesema kuwa Macron alizungumza jana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na wawili hao watazungumza tena wakati mkutano huo utakapokamilika.