1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ataka misaada ya kimataifa iingie nchini

Mtullya, Abdu Said22 Mei 2008

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aanza kutembelea sehemu zilizokumbwa na maafa yaliyosababishwa na kimbunga Nargis nchini Myanmar.

https://p.dw.com/p/E4Ec
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.Picha: AP


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameanza kuzitembelea sehemu zilizokumbwa na maafa ya kimbunga Nargis nchini Myanmar baada ya kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa nchi hiyo leo Thein Sein . Katibu mkuu Ban Ki-moon alipanda helikopta na kuanza kulitembela jimbo la Irawaddy-moja ya maeneo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa na maafa yaliyosababishwa na kimbunga Nargis kilichoikumba Myanmar wiki tatu zilizopita.

Katibu mkuu Ban Ki-moon amesema ameenda Myanmar kuwasilisha ujumbe wa matumaini kwa watu wa nchi hiyo waliokumbwa na maafa ya kimbunga ambapo hadi sasa watu wapatao 133,000 wameripotiwa kuwa wamekufa ama hawajulikani walipo. Ban Ki -moon amesema ana uhakika kuwa itawezekana kuyakabili maafa ya kimbunga kwa ufanisi.

Lakini wakati huo huo amewataka watawala wa kijeshi wa Myanmar wakubali misaada ya jumuiya ya kimataifa iwafikie watu zaidi ya milioni 2 ambao sasa hawana namna yoyote ya kujikimu.

Baadae leo katibu mkuu Ban Ki-moon anatarajiwa kukutana na wawakilishi wa shirika la misaada la msalaba mwekundu na mawaziri wa utawala wa kijeshi wa Mynamar.

Wiki tatu baada ya kimbunga Nargis kuleta maafa makubwa nchini,misaada ya kimataifa imewafikia asilimia 25 tu ya wahitaji.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa lengo la ziara yake ni kuharakisha taratibu zote ili mashirika ya misaada ya kimataifa yaweze kufanya kazi bila ya kipingamizi.

Hapo kesho, ban Ki- moon anatarajiwa kuutembelea mji mkuu mpya wa Myanmar Naypyitaw, uliopo kilometa 350 kaskazini ya mji mkuu wa sasa Yangon.

Atakutana na kiongozi wa utawala wa kijeshi Than Shwe katika mji mkuu huo mpya.

Katibu mkuu Ban Ki- moon anatazamiwa kurejea mjini Yangon jumapili ili kuongoza mkutano wa wafadhili juu mahitaji ya Myanmar ya haraka na ya muda ya mrefu.Mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe kutoka Umoja wa nchi za kusini mashariki mwa Asia Asean.