Katibu Mkuu wa NATO na Rais wa Ukraine wakutana mjini Kyiv
20 Aprili 2023Katika mkutano wao Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky waligusia masuala makuu manne ambayo ni mkutano kuhusu ulinzi wa Ukraine katika muundo wa "Ramstein" wa Aprili 21, juu ya kuwahimiza washirika kutoa aina fulani za silaha, maandalizi ya mkutano wa kilele wa NATO utakao fanyika mjini Vilnius na nne juu ya dhamana ya usalama kwa nchi ya Ukraine kuelekea kujiunga kwake na jumuiya ya NATO.
Kwenye mkutano wa pamoja na wandishi Katibu Mkuu wa NATO alisema mahala sahihi pa Ukraine ni katika familia ya nchi za Ulaya za Atlantiki na kwamba Ukraine inapaswa kuwemo kwenye jumuiya ya NATO ambapo jumuiya hiyo inafaa kuisaidia Ukraine kufanikisha hilo. Stoltenberg pia amemwalika Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwenye mkutano wa kilele wa NATO mjini Vilnius nchini Lithuania mwezi Julai, akimhakikishia kuwa jumuiya ya kijeshi ya NATO itasimama na Ukraine muda wote.
Soma:Mkuu wa NATO asema Ukraine itajiunga na jumuiya hiyo siku moja
Kwa upande wake rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema ziara ya Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg nchini mwake ni ishara kwamba jumuiya hiyo ya kijeshi iko tayari kuanza sura mpya ya maamuzi kabambe katika uhusiano wake na Ukraine.
Ujerumani imeahidi kuipa Ukraine vifafu vingine vinne aina ya Leopard 2. Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema idadi ya vifaru hivyo itaongezeka kutoka 14 hadi 18. Wakati huo huo Uswizi leo hii Alhamisi imeliongeza kundi la Wagner kwenye orodha yake ya vikwazo baada ya hatua kama hiyo kuchukuliwa na Umoja wa Ulaya wiki iliyopita.
Soma:Mkuu wa NATO azuru Ukraine kwa mara ya kwanza tangu uvamizi wa Urusi
Vikosi vya mamluki wa Wagner vimekuwa vikiongoza mashambulizi mashariki mwa Ukraine, ukiwemo mji wa Bakhmut, ambao umekumbwa na vita kwa muda mrefu na umwagikaji damu. Hata hivyo licha ya shinikizo kutoka kwa Ukraine na washirika wake, Uswisi imekataa kuruhusu nchi zinazomiliki silaha za nchi hiyo kuzipeleka nchini Ukraine.
Vyanzo:RTRE/AFP/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga