1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu wa NATO kukutana na Donald Trump

2 Aprili 2019

Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amepangiwa kukutana na rais Donald Trump wa Marekani leo mnamo wakati jumuia hiyo inajiandaa kuadhimisha miaka 70 tangu ilipoundwa.

https://p.dw.com/p/3G70n
NATO Jens Stoltenberg PK zum Ministertreffen in Brüssel
Picha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg amepangiwa kukutana na rais Donald Trump wa Marekani leo Jumanne mnamo wakati jumuia hiyo inajiandaa kuadhimisha miaka 70 tangu ilipoundwa.

Ziara katika ikulu ya Marekani, inafanyika siku mbili kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa NATO mjini Wadhington utakaogubikwa kwa mara nyengine tena na jinamizi la Urusi.

Trump, kinyume na jukumu lake kama mwanachama mwanzilishi wa jumuia ya NATO amekuwa mara kadhaa akishuku haja ya kuwa na jumuia hiyo na kufika hadi ya kuwaita washirika wake kuwa ni wadowezi tu.

Ameshawahi wakati mmoja kujiuiza kwanini NATO iihami nchi ndogo ya Montenegro na kukasirishwa kuiona Ujerumani nchi yenye nguvu zaidi kiuchumi barani Ulaya haifanyi bidii za kulifikia lengo lililowekwa na NATO la kutenga asili mia mbili za pato la ndani kwaajili ya bajeti ya ulinzi.

Stoltenberg ataka uwajibikaji wa Ujerumani

Deutschland - Merkel empfängt Nato-Generalsekretär Stoltenberg in Berlin
Picha: picture-alliance/AP/M. Schreiber

Katibu mkuu wa jumuia ya NATO, Jens Stoltenberg akizungumza na waandishi habari kabla ya kuondoka kwenye makao makuu ya jumuia hiyo mjini Brussels amekiri Ujerumani inabidi ijiambatanishe na ahadi ilizotoa mkutano wa kilele wa NATO ulipoitishwa mwaka 2014.

"Nataraji Ujerumani itajiambatanisha na ahadi ilizotoa pamoja na washirika wote wa NATO" amesema Stoltenberg ,ambnae zamani alikuwa waziri mkuu wa Norway.

"Nataraji watatekeleza ahadi walizotoa kuhusu gharama  na wameshawasilisha mpango wa kitaifa unaoonyesha jinsi Ujerumani itakavyozidisha bajeti ya ulinzi kwa kiwango cha hadi asili misa 80 ikilinganishwa na mwongo mmoja uliopita.

Balozi wa marekani katika jumuia ya kujihami ya NATO, Key Bailey Hutchison ameelezea pia matumaini kuiona serikali ya kansela Angela Markel inangeza bajeti yake ya ulinzi-matumaini hayo ameyaelezea kidiplomasia kinyume na alivyofanya rais Trump.

"Tunategemea mengi zaidi kutoka ujerumani kwasababu ni nchi yenye nguvu zaidi kiuchumi barani Ulaya.Wanabidi wawajibike zaidi na nnajua kansela Angela Merkel ana azma hiyo hiyo." amesema balozi wa Marekani katika jumuia ya kujihami ya NATO katika mkutano na waandishi habari mjini Brussels.

Suala la bajeti ya NATO pasua kichwa

Belgien Nato-Gipfel
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Kama suala la bajeti ya ulinzi linaleta mgawanyiko ndani ya NATO lile kuhusu wasi wasi kuelekea Urusi linaungwa mkono na wengi wa wanachama,kufuatia nchi hiyo kuwaunga mkono waasi katika vita vyao nchini Ukraine pamoja na kuitwaa raasi ya Crimea.

Mada zote hizo pamoja pia na hatua zinazohitajika baada ya kuvunjika makubaliano ya kimataifa yanayopiga marufuku makombora ya nuklea yanayoweza kushambulia bara moja hadi jengine zitajadilia wakati wa mkutano wa sku mbili wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje kuadhimiha miaka 70 tangu jumuia ya NATO ilipoundwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo