Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon aizuru Somalia
9 Desemba 2011Hii ni safari ya kwanza ya kushtukiza kwa kiongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo iliyogubikwa na vita kwa muda mrefu.
Ban Ki Moon amefanikiwa kufika mjini Mogadishu kutokana na mabadiliko chanya yaliyofanywa mwaka huu na Umoja wa Majeshi ya Umoja wa Afrika, AMISOM, dhidi ya wanamgambo wa Al Shabab, ambao hivi karibuni wamebadilisha jina na kujiita Imaarah Islamiya.
Licha ya jitihada zao za kuendesha kampeni ya mashambulio ya mabomu katika barabara za Mogadishu, mji ambao walikuwa wakiushikilia muda kama huu mwaka jana, ulinzi umeimarishwa katika Uwanja wa Ndege alikoshukia kiongozi huyo.
Muda mfupi uliopita, nimezungumza na mwandishi wetu Aweis Sheikh aliyeko Mogadishu juu ya ujio wa Katibu Mkuu huyo, licha ya njama za wanamgambo wa Al Shabab.
Muda mfupi baada ya kuwasili kwake, Ban Ki-Moon amekutana na viongozi wa serikali ya mpito ya Somalia na baadhi ya maofisa wa jeshi la Umoja wa Afrika, AU, na anatarajiwa kutoa tamko juu ya uhusikaji wa Umoja wa Mataifa mjini Mogadishu.
Ziara hiyo imegubikwa na usiri wa hali ya juu, na hakukuwa na taarifa yoyote kwa umma kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa angeizuru Somalia siku za hivi karibuni. Hata hivyo, minong´ono ilianza kuvuma mjini Mogadishu jioni ya jana kufuatia Moon kuizuru Kenya.
Raia wa Mogadishu walianza kushuhudia vita mnamo mwaka 1991 baada ya rais wake wa mwisho kupinduliwa madarakani. Na tangu hapo, taifa la Somalia limekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa takriban miongo miwili sasa, hali inayozidi kudidimiza uchumi wa nchi na raia kwa ujumla.
Mji wa Mogadishu hauna mabalozi wa kimataifa na unapokea misaada michache sana kutoka nchi za magharibi.
Ujio wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon unaashiria kuwa Umoja wa Mataifa inaamini kuwa licha ya changamoto zinazoikabili Somalia, jeshi la Muungano wa Majeshi ya Umoja wa Afrika AMISOM, umefanya kazi inayoleta matumaini mapya kwa Somalia.
Mwandishi: Pendo Paul
Mhariri: Othman Miraji