1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan ziarani nchini Niger

Epiphania Buzizi24 Agosti 2005

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan,yuko ziarani nchini Niger ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake inayolenga kutathimini hali ya mgogoro wa chakula nchini Niger.

https://p.dw.com/p/CHf7
Kofi Annan na mke wake Nane wakiwa katika wadi ya watoto katika Hospital ya Zinder, Niger
Kofi Annan na mke wake Nane wakiwa katika wadi ya watoto katika Hospital ya Zinder, NigerPicha: AP

Bwana Annan amesema anataraji kuzungumza na viongizi wa nchi hiyo katika kutafuta suluhisho la muda mrefu juu ya tatizo la njaa ambalo limewaathiri watu milioni tano nchini Niger.

Bwana Kofi Annan alipokelewa uwanja wa ndege na rais wa Niger Tandja Mamadou,ambaye anaulaumu Umoja wa Mataifa na mashirika ya miasaada, kwa kutia chumvi taarifa juu ya kiwango cha matatizo ya nchi yake.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alilakiwa kwa shangwe na Mamia ya wananchi ambao hata hivyo walipaaza sautu zao wakisema njaa njaa.

Ziara ya siku mbili ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Niger, inalenga kutathimini mwenyewe hali ya janga hilo ilivyo, na kushauriana na viongozi wa nchi hiyo juu ya mikakati ya pamoja ya kukabiliana na tatizo sugu la ukame.

Bwana Kofi Annan ambaye aliambatana na mke wake pamoja na ujumbe wa watu 100, aliitembelea Hospital kuu ya mji wa Zinder wa pili kwa ukubwa nchini Niger, ambayo inawatibu watoto wenye utopia mlo,na baadaye kukizulu kituo kinachotoa huduma za lishe kwa watoto katika mji huo wa Zinder.

Mwenyeji wake rais Mamadou, alikabiliwa na lawama kutoka kwa upinzani, kwamba hakutoa mwito kwenye jumuiya ya kimataifa kuomba misaada ya dharura wakati taifa lake lilipokabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula.

Leo Bwana Annan atakutana na rais Mamadou Tandja pamoja na maofisa wa serikali kuzungumzia namna ya kusaidia zaidi maeneo yaliyoathiriwa vibaya na ukosefu wa chakula.

Maafisa wa shirila la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres , ambalo mwaka huu lilitoa huduma kwa watoto wapatao elfu 21 wenye utopia mlo, katika hotuba yao kwa Bwana Kofi Annan, walisema kwamba Umoja wa Mataifa ulichelewa kutoa misaada ya chakula kwa wahitaji nchini Niger, na bado umoja huo unaendelea kutoa misaada ambayo haitoshi mahitaji ya walengwa.

Maafa ya njaa nchini Niger, ambayo yalitokana na ukamwe na uharibifu uliosababishwa na nzige, yamewaathiri watu milioni tano ambao walikabiliwa na ukosefu wa chakula.

Umoja wa mataifa unasema kwamba ungeweza kutoa misaada ya dharura kukabiliana na mgogoro huo wa njaa nchini Niger, ikiwa mataifa wahisani yange itikia haraka mwito wa msaada na kutoa fedha mwezi Mei.

Lakini maafisa wa shirika la waganga wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres, wamesema kwamba shirika la mpango wa chakula Duniani ,WFP, lilitoa misaada yake kulingana na utaratibu wake wa kawaida wa kuitoa misaada ya chakula kama malipo kwa watu wanaofanya shughuli katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji, na piakutoa misaada ya chakula mashuleni, badala ya kutoa misaada ya dharura kwa watu wenye tatizo la njaa.

Shirika la waganaga wasio na mipaka, pia limesema misaada ya dharura ya chakula haiwafikii walengwa, kwa sababu mara nyingi shirika la mpango wa chakula Duniani ,hutegemea twakwimu za mavuno kuliko kujali taarifa za watu wanaohitaji misaada zaidi.

Shirika hilo pia limedai kuwepo kwa ukosefu wa misaada ya chakula chenye virutubisho kinachowafaa watoto wenye utopia mlo.

Limeongeza kuwa, hadi sasa misaada inayotolewa na shirika la mpango wa chakula Duniani, haitoshelezi mahitaji ya watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula nchini Niger.

Shirika la wanganga wasio na mipaka linasema kiwango cha tatizo la watoto wenye utopia mlo ni cha juu, na misaada zaidi inahitajika.

Umoja wa mataifa ambao ulianza operesheni kubwa ya kutoa misaada ya dharura ya chakula mwezi huu, unalenga kutoa misaada hiyo kwa wananchi wapatao milioni mbili na nusu nchini Niger, nchi ambayo ni moja wapo ya zilizokumbwa na baa la njaa huko Afrika Magharibi. Nchi nyingine zinazokabiliwa na njaa ni pamoja na Mali, Mauritania na Burkinafaso.