Katibu Mkuu wa UN Gutteres ahimiza makubaliano COP28
11 Desemba 2023Shinikizo hilo la Guterres limekuja wakati mkutano huo wa kilele wa kimataifa ukielekea dakika zake za mwisho kabla ya kumalizika siku ya Jumanne.
Kiongozi huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema bado kuna mianya ambayo inaleta kizuizi cha kupatikana maridhiano miongoni mwa mataifa takriban 200 yanayoshiriki mkutano huo.
Nchi wazalishaji wakubwa wa mafuta na gesi zikiongozwa na Saudi Arabia zinashikilia msimamo wao kutokubaliana na mpango wa kusitisha kabisa matumizi ya nishati za visukuku.
Rais wa mkutano huo wa COP28 ambaye pia anaongoza shirika la taifa la mafuta la Umoja wa falme za Kiarabu, mara kadhaa ameahidi kwamba makubaliano ya kihistoria yatafikiwa kwenye mkutano huo, na amezitolea mwito nchi zinazoshiriki kutafuta maridhiano na msingi wa pamoja kuhusu suala hilo la nishati za visukuku.