1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa baraza la haki za binadamu wafunguliwa

26 Februari 2024

Vita vya Gaza,Sudan,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Myanmar vyagubika mkutano wa UNHRC

https://p.dw.com/p/4cuLa
Schweiz | Sitzung UN Menschenrechtsrat in Genf | Antonio Guterres
Picha: Benoit Doppagne/Belga/dpa/picture alliance

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu umefunguliwa mjini Geneva kwa kutolewa,kauli zinazoonesha namna hali inavyotisha duniani.

Vita,migogoro na mivutano ni masuala yaliyohodhi mkutano huo, huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa,Antonio Guterres akisikitishwa na namna ambavyo wanaohusika vitani wanavyofumbia macho sheria ya kimataifa.

Mkutano huo wa Kimataifa wa haki za binadamu unaitazama hali jumla inayoshuhudiwa hivi sasa ambapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hotuba yake ya ufunguzi ametahadharisha kwamba ulimwengu unaelekea kuwa sehemu isiyo salama kila siku.

Mji wa Kiev nchini Ukraine
Mji wa Kiev ulivyoharibiwa kwa vitaPicha: John Moore/Getty Images

Kwa kutambuwa hilo akatowa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kushirikiana kwa karibu badala ya kutengana na kutoa nafasi kwa mitizamo ya chuki na ukandamizaji wa haki za binadamu.

Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa hakusita kuzungumzia vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza kwa kusema sheria inayosimamia masuala ya kibinadamu inatambuwa kwamba kuhangaihswa kwa raia na kunyimwa chakula,maji na huduma ya afya ni kichocheo cha hasira zisizokuwa na mwisho,mtengano,itikadi kali na vita.Na juu ya hilo amebaini kwamba ulimwengu unashuhudia mgawanyiko mkubwa hivi sasa.

''Kuanzia Ukraine mpaka Sudan hadi Myanmar,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Gaza,pande zilizoko vitani zinafumbia jicho sheria ya kimataifa,mikataba ya geneva na miongozo ya Umoja wa Mataifa.Baraza la usalama mara nyingi linajikuta kwenye mkwamo na kushindwa kuchukuwa hatua juu ya masuala muhimu ya amani na usalama yanayoshuhudiwa kipindi hiki''

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema haki za binadamu zinashambuliwa kwa namna mbali mbali na kusisitiza miito ya kufutiwa madeni kwa baadhi ya nchi masikini na kuongezwa kwa fedha za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

 

Mkutano huo umegubikwa zaidi na vita migogoro na mivutano.Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amesema ulimwengu unashuhudia kile alichokiita zilzala iliyosababisha mshtuko mkubwa.Soma pia: UN: Ni hatari kusitisha ufadhili kwa shirika la UNRWA

Bila ya kuchuja maneno Türk amezungumza wazi wazi akisema maumivu na uchinjaji wa watu chungunzima katika mashariki ya kati,Ukraine,Sudan,Myanmar Haiti na katika maeneo mengine mengi duniani ni mambo yasiyoweza kuvumilika.Volker Türk kama Guterres amelitetea shirika la Umoja wa Mataifa linalowasaidia Wakimbizi Wapalestina UNRWA.

Ofisi za UNRWA zilivyoharibiwa Gaza
Makao makuu ya UNRWA katika mji wa GazaPicha: Karam Hassan/Anadolu/picture alliance

''Nasikitishwa sana na majaribio ya kuhujumiwa uhalali na kazi za Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi nyingine.Hujuma hizo ni pamoja na kutolewa taarifa za uwongo zinazoyalenga mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa,walinda amani wa Umoja huo na ofisi yangu. Umoja wa Mataifa umegeuka kuwa walengwa wa propaganda za hila na kutumiwa kama kisingizio cha kushindwa kwa sera. Hili ni jambo la upotoshaji wa nia njema na linalowahujumu watu wengi ambao maisha yake yanategemea mashirika ya Umoja huo''

Mtazamo huo wa Volker Türk umetolewa pia na rais wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa Dennis Francis, akisisitiza kwamba kwa kuzingatia ubinadamu, Umoja wa Mataifa unapaswa kuwa na msimamo mmoja kutumia majukwaa yao kupaza sauti kudai hatua ya kusitishwa vita mara moja katika Ukanda wa Gaza,  kwaajili ya kupelekwa misaada ya  kibinadamu na kutolewa njia kwa watu wanaohitaji msaada wa haraka wa matibabu,  kwa wapalestina milioni 1.5 walioachwa bila makaazi.

Vikao vya baraza hilo la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa vitaendelea kwa wiki sita zijazo huku wajumbe wengi wakitafakari juu ya kifo cha aliyekuwa mkosoaji mkubwa wa rais Vladmir Putin  Alexei Navalny,kilichotokea mwezi huu akiwa jela nchini Urusi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW