Katika kivuli cha Mandela: Tathmini ya ziara ya Obama Afrika
1 Julai 2013Rais mweusi sawa na rais wa Afrika?
Ziara yake kubwa zaidi barani Afrika wakati wa utawala wake - ya kwanza nchini Ghana mwaka 2009 ilidumu kwa masaa 18 - imegubikwa si tu na ugonjwa wa Mandela, ambao umeiweka Afrika kusini njia panda. Lakini rais huyo wa Marekani mwenye asili yake nchini Kenya lazima authibitishie umma uliokata tamaa kuwa analichukulia kwa uzito unaostahili bara la baba yake, kama walivyofanya watangulizi wake, Bill Clinton na George Bush. Miradi ya mabilioni ya afya na biashara ya marais hao, inaendelea kusifiwa barani Afrika. "Hata Bush amelifanyia mengi zaidi bara la Afrika kuliko Obama," kilisema kichwa cha gazeti la Afrika Kusini wakati akiwasili huko.
Maandamano dhidi ya "mvamizi Marekani"
Makundi ya wanafunzi na yale ya siasa za mrengo wa kushoto yalifanya maandamano kupinga ziara ya Obama kutokana na sera ya Marekani mashariki ya kati na kuiita nchi hiyo muuaji mkubwa wa dunia. Wakati Obama akitangaza mpango wa udhamini wa masomo ya uongozi kwa vijana 500 kila mwaka katika chuo kikuu cha Johannesburg, kulikuwapo na makofi ndani ya ukumbi. Lakini nje kulikuwa na maandamano ya vurugu, kiasi kwamba polisi ililaazimika kutumia risasi za mpira kuyatawanya.
Ilikuwa Jumapili tulivu (30.06.2013) wakati Obama alipotembelea gereza la kisiwa cha Robben, ambako Mandela alitumikia 18 ya miaka yake 27 jela. "Dunia inawashukuru mashujaa wa kisiwa cha Roben," Obama ambae alikuwa pamoja na mkewe Michelle na binti zake wawili aliandika katika kitabu cha wageni, na baadae alitembelea chumba alichofungiwa Mandela na machimbo ya mawe ya sifa mbaya.
Katikati ya misitare: Mwenyeji pia akosolewa
Jioni ya Jumapili (30.06.2013) rais huyo wa Marekani alitoa hotuba ya kuchangamsha na iliyojaa hamasa katika Chuo Kikuu cha Cape Town, ambayo ilikumbushia juu ya Obama wa wakati ule wa kugombea urais. Kwa mara ya kwanza kabisaa katika ziara yake, Obama aliweza kuwavutia Waafrika Kusini. Alinukuu katika hotuba ya Seneta Robert Kennedy miaka 47 nyuma, ambae, akiwa katika eneo hilo hilo, alifananisha harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi, na vuguvugu la Wamarekani weusi kudai haki za za kiraia nchini kwake.
Mwaka 2013 mbele ya wasikilizaji zaidi ya 1000, Obama aliwalaani Waafrika wanaotumia nguvu kuwaibia na kuwabagua wengine, matamashi ambayo yalipokelewa kwa vifijo. Kwa wanaotaka wangeweza kutafsiri matamshi ya Obama kama kumchimba pia mwenyeji wake: Rais Jacob Zuma na maafisa waandamizi wa serikali yake wanatuhumiwa kushiriki vitendo vya rushwa, sababu moja kwa nini wapiga kura katika mkoa wa Cape, tofauti na wengine nchini humo, wanakichagua chama cha Democratic Alliance (DA) badala ya chama tawala cha rais Zuma, cha Africa National Congress (ANC).
Suluhisho la Afrika kwa matatizo ya kiafrika
Obama alisisitiza katika hotuba yake umuhimu wa waafrika kubeba majukumu yao wenyewe: "Hii ni kazi ya Waafrika wenyewe." Obama alizungumzia hali nchini Zimbabwe, ambako hali mbaya ya kisiasa imesababisha kuanguka kwa uchumi. Wakati huo huo, Obama alibainisha mpango wa uwekezaji wenye thamani ya karibu euro bilioni 5.4 katika sekta ya nishati ya Afrika katika miaka mitano ijayo.
Jumatatu (01.07.) Oabama atakuwa mgeni nchini Tanzania, kituo chake cha mwishi cha ziara ya bara la Afrika. Inaweza kuwa bahati mbaya, lakini ziara ya Obama inafuatia ile ya rais wa China Xi Jinping aliezizuru nchi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali za Afrika Kusini na Tanzania mwezi Machi. China illipiku Marekani mwaka 2009, kama mshirika mkubwa zaidi wa kiabiashara wa bara la Afrika.
Madiba badala ya Obama
Mwisho wa siku ni utambuzi mchungu kwa wapanga mikakati wa ikulu ya White House kuwa mpango wa kumtabulisha Obama katika jaribio la pili kama rais wa Afrika haujafanikiwa.Hata nchini Senegal, mazungumzo yalikuwa juu ya Mandela, ambae Obama alimsifia kama "msukumo kwa ulimwengu" tena na tena. Vipaumbele vyake mwenyewe havikuweza kupata nafasi nzuri licha ya hotuba ya kuvutia mjini Cape.
Kinyume chake, akiwa mjini Dakar ugonvi haukuwa tu juu ya mada ya ushoga, mjini Cape Town ziara hiyo ilikumbwa na uhasama wa wazi kutoka muungano wa mashirika mbalimbali ya kiraia. Pia barani Afrika kuna upinzani mkubwa dhidi ya matumizi ya ndege zisizotumia rubani. Kwa hivyo ile hali ya furaha ya mwaka 2009 sasa inatishiwa na matatizo ya ajira na uwekezaji nchini Marekani. Kwa hivyo Tanzania, nchi iliyo jirani kabisaa na nchi ya asili ya baba yake Obama, ni kama kitu cha jaribio la mwisho tu.
Mwandishi: Schadomsky Ludger
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Saum Yusuf