Kazi ya sanaa za Afrika zilizoibwa wakati wa ukoloni
21 Desemba 2020Jumba la makumbusho la Humbold Forum lililofunguliwa hivi karibuni mjini Berlin, linahifadhi baadhi ya kazi za sanaa na vifaa vya kitamaduni vilivyoibiwa kutoka nchi za Afrika wakati wa ukoloni. Harrison Mwilima, ambaye ni mwandishi wetu mjini Berlin,anaona kwamba ufunguzi wa makumbusho hayo inabidi utoe chachu kwa nchi za Afrika kuuangana na kudai kurudishiwa urithi wao wa asili.
Wiki iliyopita, siku ya Jumatano tarehe 16 mwezi huu wa Disemba, jumba kubwa la makumbusho lililokuwa likisubiriwa kwa hamu la Humboldt Forum, lilifunguliwa mjini Berlin. Jumba hilo litahifadhi takribani kazi za sanaa 75,000 kutoka barani Afrika.
Hiyo ndio maana kuna nchi mbali mbali zinazodai vifaa vyao vilivyoibiwa wakati wa ukoloni. Mfano ni nchi ya Nigeria, inayodai kurudishiwa vinyago vyake vilivyoibiwa na Waingereza wakati wa ukoloni. Vinyago hivyo viliuzwa na kupita katika mikono mbali mbali na sasa baadhi yake vipo mjini Berlin na vitakuwa ni kati ya vifaa vitakavyoonyeshwa katika jumba hilo la makumbusho.
Wiki moja kabla ya ufunguzi wa makumbusho hayo ya Humboldt Forum, balozi wa Nigeria nchini Ujerumani, Yusuf Tuggar, aliiandikia barua serikali ya Ujerumani kutaka nchi yake irudishiwe vinyago hivyo. Barua hiyo ilikuwa ni ya pili baada ya barua ya kwanza aliyoituma mwezi wa Agosti mwaka jana kutojibiwa.
Mwaka jana Ujerumani ilirudisha nchini Namibia jiwe linalokadiliwa kuwepo kuwa na miaka 500. Hiyo ilikuwa ni baada ya serikali ya Namibia kuomba irudishwe jiwe hilo tangu mwaka 2017.
Ethiopia pia imekuwa ikiomba kurudishwa vitu vyao kutoka Uingereza. Nchi kama vile Benin, Senegal na Ivory Coast, pia ni kati ya nchi zinazotaka kurudishiwa vitu vyao vilivyoibiwa wakati wa ukoloni kutoka kwa wafaransa.
Madai hayo mengi yanashindwa kutimizwa kwani bado kuna utofauti mkubwa wa nguvu na ushawishi kati ya nchi hizo zilizotawaliwa na zile zilizotawala. Nchi zingine za Afrika zinaweza pia kuogopa kudai vitu vyao kwa nia ya kuzuia athari za kidiplomasia zinazoweza kutokea kama vile kunyimwa misaada ya kimaendeleo pamoja na kutoungwa mkono na nchi zilizowatawala katika jumuiya ya kimataifa.
Hiyo inafanya jitihada nyingi za kuhakikisha kazi za sanaa zilizoibiwa zinarudishwa barani Afrika, kufanyika sana barani Ulaya kupitia asasi zisizo za kiserikali, wanaharakati na watu wengine binafsi. Ni muhimu kwa serikali za nchi za Afrika pia kuhakikisha zinawezesha mchakato huo pia katika nchi zao.
Serikali za nchi za Afrika inabidi zitengenea sera maalum za kutaka kurudishiwa vitu vyao. Sera hizo inabidi pia zihusishe jumuiya zao za kikanda.
Kwa mfano nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaweza kutengeneza sera katika nchi zao na baada ya hapo nchi hizo zinaweza kuja pamoja na kutengeneza sera ya kanda nzima kwa ajili ya kuhakikisha vitu vilivyoibiwa kutoka kanda hiyo vinarudishwa.
Baada ya kanda za Afrika kutengeneza sera zao, jumuiya zao zinaweza ungana pamoja kupitia Umoja wa Afrika na kutengeneza sera ya bara zima kwa ajili ya kuweka msukumo wa kurudisha vitu vilivyoibiwa.
Sera ya Umoja wa Afrika inayotoa maono ya kufikiwa mpaka mwaka 2063, inaonyesha kwamba mkakati wake nambari tano ni kufanya bara la Afrika kuwa na utambulisho wa kipekee. Kati ya vitu hivyo ambavyo vinaweza pelekea kuleta utambulisho huo ni utamaduni wa kiasili kupitia kazi mbali mbali za sanaa, ambazo kwa kiasi kikubwa zipo katika makumbusho tofauti barani Ulaya na zinaendelea kunufaisha miji hiyo ya Ulaya kiuchumi.
Swali ni je ni waafrika wangapi wanaoweza kufunga safari kuja kwenye jumba la makumbusho la Humboldt Forum la Berin kujifunza kuhusu utambulisho na urithi wao wa kitamaduni?
Nchi za kiafrika zina wajibu mkubwa wa kuja na mikakati maalum pamoja na kuungana ili kufanikisha urudishiwaji wa vitu vyao vya asili.
Mwandishi: Harrison Mwilima
Mhariri: Gakuba, Daniel