Kenneth Kaunda afariki dunia
17 Juni 2021Mwasisi wa taifa la Zambia kenneth Kaunda amefariki dunia. Kaunda amefariki akiwa anapatiwa matibabu ya maradhi ya nimonia akiwa na miaka 97.
Watoto wake wa kiume Panji na Kambarage Kaunda wamelithibitishia shirika la habari la DPA kuhusu kifo hicho hii leo.
Siku tatu zilizopita Kaunda alikuwa amelazwa katika hospitali ya kijeshi mjini Lusaka. Maafisa hata hivyo hawakuweka wazi maradhi yaliyokuwa yakimsumbua, lakini yalibainika wakati taifa hilo la kusini mwa Afrika likishuhudia kuongezeka kwa maambukizi ya maradhi ya COVID-19.
Kaunda alikuwa akichukuliwa kama mmoja ya manusura wa mwisho miongoni mwa kundi la mashujaa wa uhuru barani Afrika. Alitawala Zambia kuanzia mwaka 1964 hadi 1991.
Akiwa madarakani, Zambia lilikuwa taifa lililoongozwa chini ya mfumo wa chama kimoja, hatua iliyompa mamlaka makubwa ya kulidhibiti taifa hilo.
Kaunda anasifika kwa kujenga shule na hospitali, tofauti na serikali za kikoloni ambazo ziliwekeza kidogo mno kwenye sekta hizo. Baada ya kustaafu na kuachana na siasa, Kaunda alijiingiza kwenye shughuli za misaada ya kiutu kupitia wakfu wake wa Kenneth Kaunda Children of Africa, inayojishughulisha na masuala ya janga la virusi vya UKIMWI.